Naibu Waziri Chumi atembelea Maonesho ya Nanenane 2025 atoa wito kutumia teknolojia kuibua Kilimo
Na. Mwandishi wetu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ametembelea Maonesho ya ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma. Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya washiriki, Chumi alisema ameridhishwa na ubunifu, teknolojia bunifu na ushiriki mpana wa wadau kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wajasiriamali, taasisi za utafiti, mashirika ya kimataifa na wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. “Maonesho haya ni jukwaa muhimu sana siyo tu kwa kukuza sekta ya kilimo, bali pia kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia uhamasishaji wa bidhaa na teknolojia bora za Kitanzania kupata masoko ya kimataifa,” alisema Chumi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutumia maonesho hayo kama fursa ya kubadilishana maarifa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi...