Hombolo Satellite City kuibadilisha Dodoma, mradi wa mji wa kisasa wachukua sura mpya

Na. Coletha Charles, DODOMA

Jiji la Dodoma linatarajia kupata sura mpya kupitia mradi wa Mji wa Kisasa wa Hombolo (HOTSAC), kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa upembuzi yakinifu na uandaaji wa Mpango Kabambe.



Mkataba huo umesainiwa Chinangali Park, Kata ya Chamwino, jijini Dodoma, katika hafla iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa, viongozi mbalimbali, wawekezaji na wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa utekelezaji wa mpango huo utakuwa chachu ya mabadiliko makubwa yatakayoiwezesha Dodoma kuendana na hadhi yake kama makao makuu ya nchi.

Alisema kuwa maandalizi yaliyoanza mwishoni mwa mwaka 2024 yalihusisha tafiti na ziara za mafunzo katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Korea, hatua iliyoongeza uelewa na uwezo wa wataalamu wa ndani.



Alisema kuwa sekta binafsi itakuwa mhimili wa utekelezaji, huku taasisi za fedha zikionesha mwitikio mkubwa wa kushiriki katika uwekezaji na kufadhili fursa zitakazotokana na mpango huo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Mji wa kisasa wa Hombolo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Azor William alisema kuwa wazo hilo limechochewa na kasi kubwa ya ukuaji wa jiji.

 

Alisema kuwa kuhamia kwa Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kumeongeza mahitaji ya ardhi, makazi, biashara na huduma mbalimbali, hivyo kuhitajika eneo litakalokidhi mahitaji hayo ya baadaye.

William alisema kuwa Hombolo inalenga kuwa kitovu cha utalii kupitia dhana ya ‘Country within the City na Global Village’, zitakazokusanya vivutio vya Tanzania pamoja na tamaduni za mataifa mbalimbali.



Nae, Mkazi wa Mtaa wa Zepisa, Kata ya Hombolo Makulu, Emmanuel Mlemeta aliishauri Serikali kuongeza juhudi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati na wananchi wananufaika na fursa zitakazotokana na Mradi huo.

Mradi huo utazingatia maendeleo endelevu na mahitaji ya vizazi vijavyo, huku wananchi wa kata tano zinazohusika wakitarajiwa kutoa maoni na kushiriki katika maandalizi ya mpango kabambe wa Mradi huo.

Comments

Popular Posts

KATA YA CHAMWINO YATEKELEZA AGIZO LA USAFI WA MAZINGIRA

Agenda ya Lishe yaongeza Ari ya usomaji S/M Dodoma Makulu

KATA YA CHAMWINO YATOA ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA