Wafugaji wahamasishwa kutumia Mbegu bora za Malisho ili kuleta tija kwenye mifugo

Na. Hellen Minja, DODOMA RS


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepiga hatua katika kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za malisho ya kupandwa (majani) yanayoleta tija kwa wafugaji kutokana na kuifanya mifugo kuwa na uzito mkubwa unaoongeza thamani yake sokoni na kuthibitisha kaulimbiu ya 'Ufugaji ni utajiri'.



Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, aliposhiriki Maonesho ya Gwaride (Paredi) la Wanyama lililofanyika kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma sanjari na Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2025 Kanda ya Kati.


“Sasa hivi wafugaji wameanza kuelewa umuhimu wa kutumia majani ya kupandwa kwa ajili ya mifugo au malisho, hatua hii ni kubwa na tunaipongeza sana na sasa tumeona wizara imepanga kuendeleza upatikanaji wa mbegu bora. Yote haya yanafanywa ili wafugaji waweze kupata uwezeshaji” alisema Senyamule.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede alitoa wito kwa wafugaji na wavuvi kwa niaba ya wizara yake, kuchangamkia fursa za matumizi ya teknolojia zinazooneshwa kwenye maonesho ya mwaka 2025 ambazo zimeendelea kusanifiwa na wataalam ili mwakani sekta hiyo iweze kuja na matokeo makubwa zaidi.




Hata hivyo, Mdhamini Mkuu wa Gwaride hilo mwaka huu, Benki ya TCB, ikiwakilishwa na Frank Kipalamoto kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, alisema kuwa taasisi hiyo imedhamini kuletwa kwa vijana 150 kutoka mikoa 12 ya Tanzania ambao ni wafugaji wa Kuku kwa lengo la kujifunza ufugaji wa kisasa utakaowaongezea tija pindi watakaporejea kwao.

Akizungumzia Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo kwa Mifugo, Dr. Benezet Lutege alisema kuwa serikali imeridhia jumla ya shilingi bilioni 216 kwa ajili ya kuendesha kampeni hiyo na utambuzi wa mifugo nchi nzima. Alisema kuwa takribani ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17 pamoja na kuku milioni 40 zitapatiwa chanjo hiyo na mifugo zaidi ya 1,000 ikiwa imeshachanjwa viwanjani hapo.

Gwaride la Mifugo mwaka 2025 ni la 14 tangu kuasisiwa kwenye kilele cha Maonesho ya Nanenane 2010, likilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia.

Comments

Popular Posts

Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini ni nyenzo ya utendaji kazi serikalini – Dkt. Biteko

JIJI LA DODOMA KUPELEKA MIL 50 ZAHANATI YA KIKUYU

WENZA WA VIONGOZI WASHAURIWA KUANZISHA BUSTANI ZA NYUMBANI