Naibu Waziri Chumi atembelea Maonesho ya Nanenane 2025 atoa wito kutumia teknolojia kuibua Kilimo
Na. Mwandishi wetu,
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi kwa
niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi
Mahmoud Thabit Kombo, ametembelea Maonesho ya ya Kilimo (Nanenane)
yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya washiriki, Chumi alisema ameridhishwa na ubunifu, teknolojia bunifu na ushiriki mpana wa wadau kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wajasiriamali, taasisi za utafiti, mashirika ya kimataifa na wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
“Maonesho
haya ni jukwaa muhimu sana siyo tu kwa kukuza sekta ya kilimo, bali pia
kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia uhamasishaji wa bidhaa na teknolojia
bora za Kitanzania kupata masoko ya kimataifa,” alisema Chumi.
Aidha,
alisisitiza umuhimu wa kutumia maonesho hayo kama fursa ya kubadilishana
maarifa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuendeleza sekta
ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa ufanisi na tija zaidi.
Katika mazungumzo na baadhi ya washiriki, wamejadili changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji, ikiwemo ukosefu wa mitaji, ukosefu wa dhamana za kiuchumi, masoko ya uhakika, pamoja na hitaji la uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo.
Chumi
alisisitiza kuwa majadiliano hayo yanaendana na mwelekeo wa Serikali wa kufikia
maendeleo ya uchumi wa viwanda, ustawi wa wananchi, na kujenga jamii yenye
uwezo wa kuzalisha kwa tija kupitia sekta za uzalishaji mali.
Maonesho
ya Nanenane hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe Mosi hadi Nane Agosti,
yakikutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali zinazohusiana na kilimo, mifugo na
uvuvi. Kaulimbiu ya maonesho kwa mwaka 2025 inasisitiza umuhimu wa uongozi bora
katika maendeleo, ikisema “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.
Comments
Post a Comment