Na. Abdul Juma, DODOMA MAKULU Mkopo wa mapato ya ndani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma usio na riba wa shilingi 328,800,000 umewawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi katika kata ya Dodoma Makulu. Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Dodoma Makulu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sophia Abdallah alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mikopo ya mapato ya ndani iliyokopeshwa kwa wanavikundi wa kata hiyo kwa kipindi cha serikali ya awamu ya sita. Alisema kuwa serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka minne imewezesha vikundi vya wanawake 21, vikundi vya vijana vitatu na vikundi vya watu wenye ulemavu sita kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao. Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa fursa kwa vijana kufanya biashara mbalimbali katika kata hiyo. “Baadhi ya vikundi vimeweza kununua bajaji na pikipiki ili kufanya biashara ya usafirishaji wa abiria kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma kwenda Sabasaba. Eneo la mare...