Teknolojia Bunifu ya Mifugo yasogezwa maonesho ya Nanenane
Na. Husna Rajabu, DODOMA
Taasisi ya Wakala wa vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA)
imeteka umakini wa wageni katika maonesho ya Nanenane jijini Dodoma kwa
kuonesha teknolojia bunifu zinazolenga kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na
kuboresha maisha ya wafugaji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Huduma za Ushauri (LITA), Joseph Msemwa, alisema kuwa taasisi hiyo imeweka bayana bidhaa na huduma kadhaa ambazo ni matokeo ya kazi za vijana wa kitanzania.
Alisema kuwa maonesho ya Nanenane ni sehemu muhimu ya
kuonesha bidhaa na teknolojia zitakazobadilisha taswira ya uchumi wa wananchi. “Tupo
hapa kwenye maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, tumeleta teknolojia mbalimbali
zinazohusiana na bidhaa za maziwa. Pia tuna teknolojia ya uchakataji wa ngozi
ambapo tunawafundisha vijana wetu namna ya kuchakata ngozi, kuanzia ikiwa
mbichi mpaka ifike hatua ya mwisho ya utengenezaji wa bidhaa. Kama mnavyojionea
bidhaa za ngozi zipo za aina tofauti tofauti ikiwemo viatu, hereni na mikanda” alisema
Msemwa.
Pia alieleza kuhusu teknolojia ya maziwa wanayofundisha
kuwa ina faida kubwa kwa wafanyabaishara na wajasiriamali. “Tunachakata maziwa
na kuongeza thamani yake, tunatengeneza maziwa mtindi, mtindi yogati na siagi. Tunatoa
mafunzo ya kufanya shughuli hiyo kwa vijana wetu ili wapate ujuzi na
kujitegemea kiuchumi” alisema.
Moja ya kivutio kikubwa ni mashine ya kutotolesha
vifaranga iliyobuniwa na vijana wa taasisi ya (LITA) wakiwa chuoni na
inapatikana kwenye maonesho ikitarajiwa kusaidia wafugaji wadogo na wakubwa.
Aidha, (LITA) imeleta teknolojia ya mfumo wa uchakataji
wa mbolea inayotokana na mifugo kama ng'ombe, mbuzi au kuku kwa lengo la
kuzalisha nishati. “Teknolojia hii inaitwa ‘biogas’. Ni teknolojia inayobebeka,
unaweza kuhamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine, na inaweza kutumika
mashambani na kwenye matumizi ya nyumbani” alieleza Msemwa.
Nae, Mkufunzi wa Chuo cha Mifugo, Joyce Balabala alizungumzia
kuhusiana na ufugaji wa sungura. “Vijana wetu tunawaelekeza namna ya ufugaji
sahihi wa sungura na jinsi ambavyo sungura wanaweza kuzalisha vitu mbalimbali.
Kwa mfano kupitia sungura unaweza kupata nyama iliyo nzuri na bora lakini pia
tumegundua mkojo wa sungura unatumika kwaajili ya mbolea” alisema Balabala.
Aidha, aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa
maandalizi ya maonesho ya Nanenane. “Maandalizi ya mwaka huu ni mazuri zaidi,
nimejaribu kuangalia kwenye mabanda mengine nimeona watu ni wengi na maandalizi
ni ya hali ya juu.
MWISHO
Imehaririwa
na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment