Elimu ya Lishe inapatikana Banda la Nanenane Jiji la Dodoma
Na. Mwanaidi Masudi, DODOMA
Mjasiriamali
kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Agnes Kinyaii, ametoa elimu ya kina
kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa wananchi waliojitokeza kwenye maonesho ya
Nanenane kitaifa yanayofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza
katika banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Kinyaii aliwasisitiza wananchi
kuzingatia ulaji wa lishe bora kama utumiaji wa viazi vya ‘bitreat’ vinavyosaidia
mambo makuu manne kuongeza damu, kukinga maradhi ya damu na afya ya mifupa ya
meno.
Aliendelea
kuelezea kuwa upo unga wa lishe uliotengenezwa katika utaratibu ambao unampatia
mtu virutubisho zaidi ya kushiba. “Kwamba tumechanganya vitu vikuu vinne,
tumeweka mahindi lishe na viazi lishe, mbegu nyeusi za maboga. Lakini pia
tumeweka ‘Almond’ na ngano isiyo kobolewa. Kwahiyo, huu unga anatumia mtoto
mdogo anayeanza kula mpaka mzee na ukila hauwezi kukuzidi nguvu kwasababu
hatujazidisha wanga. Tumeweka vitu viwili vinavyotoa wanga yaani viazi na
mahindi lishe ambayo yana viwango vikubwa vya Vitamin A zaidi hata ya wanga. Kwahiyo,
mtu anayetumia huu unga anakuwa na Vitamin A pamoja na wanga ndio maana
tunasema hiki ni chakula anatumia mtoto mpaka mtu mzima” alieleza Kinyaii.
Wakati
huohuo, alielezea zao la mwani kuwa ni zao la baharini ambalo hupatikana maeneo
ya fukwe za bahari kama Tanga, Bagamoyo, Dar es Salaam na Pwani kwa sababu linapenda
maji ya chumvi. Ni moja ya zao lenye virutubisho vingi vinavyohitajika kwenye
mwili wa binadamu wenye madini 72.
Vilevile,
aliendelea kuonesha wananchi bidhaa mbalimbali wanazotengeneza za lishe
hususani unga wa lishe ambao unawasaidia mama wanaonyonyesha kuongeza kiwango
cha maziwa. “Uji huu tumeweka mbegu nyeusi za maboga, mbegu hizo zimetengenezwa
mahususi kwa ajili ya kuchochea utengenezaji wa maziwa kwa kina mama. Kwahiyo,
yule anayenyonyesha akitumia huu uji anakuwa anapata maziwa mengi sana, wamama
wengi wanapata changamoto za kunyonyesha watoto wao kwa sababu unakuta
akishamnyonyesha mtoto wake anakaukiwa maziwa. Lengo ni kuhakikisha hakuna
mtoto ambaye anaanzishwa kula kabla hajafikisha miezi sita, mama anayenyonyesha
akitumia huu uji wetu anakuwa anapata maziwa mengi na ya uhakika wa
kumnyonyesha mtoto wake miezi sita mfululizo bila kumpa chakula chochote. Ninawasihi
sana kina mama wanaonyonyesha watoto walioko katika Jiji la Dodoma wafike
katika banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma waweze kujipatia uji huu,
tunasema mtoto akinyonya maziwa ya mama anakuwa na akili” alisema Kinyaii.
MWISHO
Comments
Post a Comment