Wasimamizi Wasaidizi Uchaguzi wapewa Semina Dodoma
Na. Dennis Gondwe, DODOMA Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata wametakiwa kusoma katiba, sheria na miongozo inayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Msisitizo huo ulitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Dodoma Mjini na Mtumba, Wakili Cosmas Nsemwa wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Alianza kwa kuwapongeza washiriki wa mafunzo kwa kuteuliwa kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata. “Someni kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na ulizeni maswali ili mpate kufafanuliwa kwenye maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine pengone yatakuwa na changamoto za kufahamu ili kuwarahisishia katika utekelezaji wenu wa kazi za uchaguzi” alisema Wakili Nsemwa. ...