Wananchi wa Hombolo wafurahia ujio wa mji wa kisasa
Na. Coletha Charles, DODOMA
Wananchi wa Kata ya
Hombolo, jijini Dodoma, wameeleza matumaini makubwa kuhusu Mradi wa Mji wa
Kisasa wa Hombolo (HOTSAC), wakiamini kuwa utachochea ukuaji wa uchumi, kuongeza
ajira na kuharakisha maendeleo ya eneo hilo.
Wakizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa Mpango Kabambe wa HOTSAC, iliyofanyika Chinangali Park, Kata ya Chamwino, wananchi hao walisema wanatarajia kunufaika na fursa zitakazotokana na mradi huo.
Diwani wa Kata ya
Hombolo Bwawani, Asedi Ndajiro alisema kuwa wananchi wamekuwa na matarajio
makubwa ya mradi huo kwa muda mrefu, wakiamini kuwa utasaidia kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili.
Alisema kuwa mradi huo
unatarajiwa kufungua fursa za ajira na kuharakisha maendeleo ya eneo hilo, huku
wananchi wakisubiri kwa hamu kuanza kwa utekelezaji wake.
Aliongeza kuwa ni
muhimu wananchi washirikishwe katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha
wanapata nafasi ya kunufaika na fursa zitakazojitokeza katika hatua mbalimbali
za maendeleo.
Kwa upande wake, mkazi
wa Mtaa wa Hombolo Bwawani B, Helena Mgonela aliishukuru Serikali inayoongozwa
na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuileta fursa hiyo katika eneo la Hombolo.
Alisema kuwa wananchi
wameupokea mradi huo kwa furaha na matumaini, huku akiutakia mafanikio ili
utekelezwe kwa kuzingatia mipango iliyowekwa na hatimaye kuleta maendeleo kwa
wakazi wa eneo hilo.
Naye mkazi wa Mtaa wa
Zepisa, Kata ya Hombolo Bwawani, Zakaria Sajiro alisema kuwa mradi huo ni fursa
muhimu inayotarajiwa kubadilisha maisha ya wananchi wanaozunguka eneo hilo.
Alisema kuwa matarajio
yao ni kuona wananchi wa kawaida wakiguswa na kunufaika na maendeleo
yatakayotokana na mradi huo, huku akieleza kufurahishwa na hatua iliyofikiwa
katika maandalizi yake.
Kwa ujumla, wananchi
hao wameeleza matumaini kuwa utekelezaji wa HOTSAC utaleta mageuzi makubwa
Hombolo, kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha maisha yao, huku wakisisitiza
umuhimu wa kushirikishwa na kunufaika moja kwa moja na maendeleo
yatakayopatikana.
MWISHO

Comments
Post a Comment