Kata ya Chamwino yatekeleza agizo la RC la usafi wa Mazingira

KATA ya Chamwino imetekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule la kufanya usafi kila jumamosi kwa lengo la kuliweka Jiji la Dodoma safi. Akiongelea utekelezaji wa agizo hilo, Afisa Mtendaji Kata ya Chamwino, Lucas Nkelege alisema kuwa usafi huo ulifanyika katika maeneo ya korongo la Mailimbili na Mwaja. Usafi huo ulihusisha kufyeka vichaka na nyasi, kuokota makopo na mifuko ya plastiki iliyozagaa katika korongo na kuzibua mitaro ya maji yenye urefu wa mita 100, aliongeza. Alisema kuwa kata yake ilitumia zoezi hilo la usafi wa pamoja kuwahimiza wananchi kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya biashara na makazi pamoja na kuhakikisha wanatunza mazingira katika msimu huu wa sikukuu. Usafi wa pamoja katika Kata ya Chamwino ulishirikisha Afisa Mtendaji Kata, Wenyeviti wa mitaa, mabalozi na wananchi.