Jiji la Dodoma lajipanga kung’ara kwa usafi, Bilioni tatu yatengwa kwaajili ya miundombinu ya taka
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira na afya za wakazi wake baada ya kuweka mpango mkakati wa kutenga shilingi bilioni tatu katika bajeti mpya ya fedha ijayo kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa taka. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mpango huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alisema kuwa bajeti hiyo inalenga kulifanya Jiji la Dodoma kuwa miongoni mwa majiji safi nchini kwa kuweka mifumo rafiki na ya kisasa ya kushughulikia taka. Alieleza kuwa fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani , jambo linaloonesha uwezo wa jiji kujitegemea katika kugharamia miradi ya maendeleo. “Suala la usafi wa mazingira halikwepeki na sisi tunasema kuwa haitawezekana kuwa na jiji chafu. Kwenye bajeti yetu mpya tumetenga takribani shilingi bilioni tatu kwaajili ya kuhakikisha vifaa vyote vya kukusanyia taka vinapatikana ” alisema Chaula. Katika utekelezaji wake, jij...