Elimu ya unyonyeshaji sahihi yatolewa kwa kina mama Jiji la Dodoma
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Akina
mama wamepewa elimu ya unyonyeshaji sahihi maziwa ya mama kwa lengo la
kuwajengea uelewa mpana utakaowasaidia kuwakuza vizuri watoto wao ili wawe na afya
njema na lishe bora katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Afisa Muuguzi Msaidizi, Kituo cha Afya Makole, Christopher Tarimo akielezea njia sahihi ya kumshika mtoto wakati wa kumnyonyesha maziwa ya mama
Hayo
yalisemwa na Afisa Muuguzi Msaidizi, Kituo cha Afya Makole, Christopher Tarimo,
alipokuwa akitoa elimu ya namna sahihi ya kumnyonyesha mtoto na lishe kwa akina
mama waliojifungua katika wodi ya wazazi kituoni hapo.
Akizungumza
na akina mama hao Afisa Muuguzi Msaizidi, aliwashauri kuzingatia mikao ya
unyonyeshaji pindi wanapowanyonyesha watoto wao. “Katika unyonyeshaji lazima
tutenge muda, ile nusu saa ya kwanza au lisaa limoja hakikisha kwamba simu
umeweka pembeni, hausumbuliwi na mtu yeyote unakuwa umetulia mawazo yote kwa
mtoto. Unatakiwa uwe umekaa, tunashauri sana kumnyonyesha mtoto ukiwa umekaa,
hakikisha umekaa mkao ambao upo ‘comfortable’ kwamba umeridhika,
mgongo wako umekaa sehemu ambapo hautadondoka, hakikisha kichwa cha mtoto wako
kipo kwenye kiwiko, hakikisha tumbo la mtoto na lako yanatazamana na
unahakikisha mtoto anakuangalia na wewe unamuangalia usoni. Kwasababu gani
tunasema hivyo, ili uweze kuona ameshika chuchu vizuri, uwe makini je, mtoto kapaliwa,
au mtoto anasinzia” alishauri kwa msisitizo Tarimo.
Akiongelea
ushikaji sahihio wa mtoto wakati wa kunyonyesha alisema kuwa ili mtoto anyonye
vizuri anatakiwa kushikwa vizuri asiweze kupaliwa na maziwa na kumfanya
ashindwe kunyonya.
“Ukimnyonyesha
mtoto hakikisha vidole vinne vinakuwa chini ya titi na ile alama nyeusi ya chuchu
yote inazama mdomoni. Chuchu ikizama mdomoni hautosikia sauti kama ya mguno,
usiposikia hiyo sauti hapo mtoto wako ananyonya vizuri na hanyonyi hewa. Na
hakikisha kwenye ziwa moja, mtoto ananyonya si chini ya dakika 30. Tunasema
hivyo, kwa sababu maziwa yamegawanyika, kuna maziwa ya mwanzo, kati na mwisho. Kwahiyo,
ukimnyonyesha ndani ya dakika 10 na ukamtoa atakuwa amenyonya maji, yale maziwa
yenye virutubisho hatoyapata” alisema Tarimo.
Vilevile,
alikwakumbusha akina mama kuzingatia mlo kamili ili kumkinga mtoto na magonjwa
yatokanayo na lishe duni kama udumavu wa mwili na akili, uzito kupita kiasi na
ukondefu.
“Naomba
niwakumbushe swala zima la mlo, mtoto anakula kupitia mama, yaani wewe
usipokula mtoto nae hali. Kwasababu, kile unachokula ndicho kinachoenda
kumeng’enywa ndani ya mwili, baadhi kinachukuliwa kinapelekwa kwenye maziwa. Kwahiyo,
hakikisha unapokula milo yako asubuhi, mchana na jioni, hiyo milo iwe ya
kukusaidia wewe kupata virutubisho kwa mtoto” alisisitiza Tarimo.
Kwa
upande wake Gladness Mauki, mkazi wa Chidachi alisema amefurahishwa kukutana na
mafunzo hayo ya lishe kwa mtoto na mikao sahihi ya kumnyonyesha pia kwasababu
hakutegemea. Alitoa rai kwa akina baba kuwa mstari wa mbele kuwasaidia kina
mama katika kukumbushana namna sahihi ya kutoa malezi bora kwa mtoto. “Leo
nimekuja kliniki, sikujiandaa kukuta mafunzo yaliyokuwa yanaendelea,
nimeshangaa tu kukuta akina mama wengi. Sana sana nimejifunza mtoto anatakiwa
kuanza kula chakula mara baada ya kufikisha miezi sita lakini nimejifunza
anapofikisha hiyo miezi sita, sio lazima kumpa mtoto chakula kingi hapo
mwanzoni ila unaweza kumpa mtoto chakula taratibu. Pia nimejifunza namna nzuri
ya kumnyonyesha mtoto, muda ambao mtoto anatakiwa kunyonya uwe ni kiasi gani. Napenda
niwashukuru kwa kutoa huduma hii na niwashauri pia watoa mafunzo wasiache kuja
mara kwa mara maana tunapata mafunzo yanayotusaidia katika malezi ya watoto.
Pia akina baba wasiache kuwasindikiza kina mama kuja kliniki ili kuweza kuwa ‘support
Psychologically’ kutoa msaada wa hapa na pale, baba anaweza akawa ni mtu wa
karibu atakayeweza kumpatia msaada mkewake” alisema Mauki.
Nae
Kurwa Kajoro, mkazi wa Michese alitoa rai kwa akina baba wenzake kuhudhuria
kliniki na akina mama ili nao waweze kuelewa kinachoendelea na kuweza
kuwakumbusha kina mama katika utekelezaji wa malezi bora kwa watoto. “Wito
wangu kwa kina baba, ninaposema kliniki ya mama, baba na mtoto ni muhimu kwa
wazazi wote sio kwamba tunamuachia anakuja mama tu. Mfano, kwa mafunzo
tuliyoyapata leo kwa wataalamu kutoka Kituo cha Afya Makole, ni kwamba tunaweza
kusaidia, mama anapokuwa amesahau yale ambayo umeyasikia unaweza
kumkumbusha na kufanya mkawa na malezi
bora kwa watoto” alisisitiza Kajoro.
Maziwa
ya mama ni lishe bora kwa mtoto, hivyo kunyonyesha sio tu husaidia kuwa na
mahusiano mazuri kati ya mama na mtoto bali ni manufaa kwa afya ya mama
yakitajwa kuwa na faida kadha zikiwa ni pamoja na maziwa kuwa kiungo muhimu kwa
maendeleo ya afya, virutubisho bora kwa mtoto anayekua, kumsaidia kujikinga dhidi
ya magonjwa, kuzuia unene wa kupindukia utotoni na kuongeza uwezo wa utendaji
kazi wa ubongo na kupunguza hatari ya kansa na magonjwa mengine.
MWISHO
Comments
Post a Comment