Vipaumbele 13 vya mageuzi elimu msingi na sekondari 2024/2025
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa mwaka 2024/25 imepanga kutumia shilingi trilioni 1.02 ili kutekeleza vipaumbele 13 kwenye sekta ya elimu vinavyolenga kusimamia na kuendesha elimu msingi na Sekondari. Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka huo, Waziri wa Nchi, TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema fedha hizo zitajenga vyumba vya madarasa 6,357, matundu ya vyoo 1,482, umaliziaji wa mabwalo 362 kati ya mabwalo hayo 15 ni msingi na 347 ni ya sekondari na umaliziaji mabweni 36 kwenye shule za awali na msingi. Pia alisema shule mpya 184, nyumba za walimu 184 na mabweni 186 katika shule za sekondari yatajengwa, sambamba na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwenye shule za awali tatu, msingi 400 na shule za sekondari 500, ununuzi wa kemikali za maabara katika shule mpya 234. Mchengerwa alisema fedha hizo zitatumika katika utoaji wa ruzuku ya elimu bila ada kwa shule za msingi 17,986 na sekondari 4,894; ununuzi na usambazaji wa vita...