TAKUKURU yapewa rai kuboresha mikakati ya kutokomeza rushwa
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU)
imeeleza kuwa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania imejipanga
kutoa elimu na kusisitiza wananchi kuepuka kupokea rushwa kwaajili ya kuchagua
viongozi.
Hayo yalielezwa na Mratibu wa Banda la TAKUKURU, Suzana Raymond wakati akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma aliyetembelea banda hilo katika maonesho ya wakulima Nanenane yanayoendelea Nzuguni jijini Dodoma.
Alisema kuwa banda la TAKUKURU limejikita katika kutoa elimu na
kupokea taarifa zinazohusu masuala ya rushwa. “Pamoja na majukumu yote, wakati mwingine tunapokea
ushauri mbalimbali kwasababu sisi tunaweza tusione tunachokifanya lakini walio
nje ndio wanaona nini tunakifanya na huwa tunapeleka ngazi za juu na wao
wanazifanyia kazi kwa kadri inavyotakikana” alisema Raymond.
Alisema kuwa lengo la kuwepo katika maonesho ya Nanenane ni
kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii hasa kuelekea uchaguzi mkuu.
“Lakini katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu tunatumia fursa hii
kuwaelimisha wananchi juu ya athari za kuchagua viongozi baada ya kupokea
rushwa. Kupitia maonesho haya tuna uelimishaji wa nje ambao wenzetu wapo
wanazunguka sehemu mbalimbali huko nje ili kuendelea kutoa elimu na kuhakikisha
suala la rushwa linatokomezwa” alimalizia Raymond.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj. Jabir Shekimweri alianza kwa kuipongeza TAKUKURU kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha mapambano ya kutokomeza rushwa yanafanikiwa. “Rushwa ipo kwenye historia ya dunia, lakini ninyi mnapaswa kuendelea na mapambano na kuhakikisha rushwa inatokomezwa kwa kubadilisha mbinu za ufanyaji kazi. Mapambano hayo yasiishie kwenye watu wazima walio makazini tu bali mbinu nyingine mbadala zitumike ili kuhakikisha suala hili linabaki historia” alisema Alhaj. Shekimweri.
Alimalizia kwa kutoa rai kwa TAKUKURU kuhakikisha
wanabadilisha mbinu na mazingira ya ufanyaji kazi. “Jambo la kwanza, nashauri
kuwa ni muhimu kuhakikisha rika dogo wanapewa elimu ya kutosha ili wakue na
mkakati huo utakaowajengea mzizi wa uzalendo mapema. Jambo la pili kuhakikisha
kuwa rika la utegemezi ambalo baada ya muda wanaingia kwenye mazingira ya elimu
ya juu na ajira wanajengewa uwezo wa nidhamu katika fedha, katika kujitegemea
na kuwajibika ili wanapoingia kazini suala la rushwa lisiwe tatizo tena. Kwenye
uchaguzi tunawategemea sana kuwa mtafanya vizuri zaidi ili kuepusha makovu
yatakayoachwa baada ya uchaguzi” alimaliza Alhaj. Shekimweri.
Maonesho
ya Nanenane kitaifa yapo katika siku yake ya sita katika viwanja vya Nanenane,
Nzuguni yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Chagua viongozi bora kwa maendeleo ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi”
MWISHO
Comments
Post a Comment