Vipando bustani vya Jiji la Dodoma yamvutia DC, Dkt. Mashinji


Na. Nancy Kivuyo, DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dkt. Vincent Mashinji ametembelea banda la vipando bustani ya mbogamboga la Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kujionea aina mbalimbali za mboga na matunda zilizoandaliwa kwaajili ya kutolea elimu na kuhamasisha wananchi kuzingatia mlo kamili.


Teknolojia hizo za kisasa zinawezesha mbogamboga kupandwa kwenye vitu mbalimbali kama kiroba, kopo la maji au eneo dogo kutokana na ufinyu wa maeneo na zikaendelea kustawi kwa ubora unaotakiwa.

Baada ya kupewa maelezo ya kina kuhusiana na aina mbalimbali za teknolojia ya upandaji wa mbogamboga alisema kuwa anawapongeza wataalam kwa kubuni njia za kisasa za kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya njema. Hiki kilimo cha mjini mnapaswa kukiangalia kwa jicho la ziada kwa kuhakikisha mnatoa elimu nzuri zaidi, lakini pia mshirikiane na watu wa mipango miji ili kuhakikisha watu wanapata maeneo mazuri yenye nafasi ya kufanya hiki mnachowaelekeza” alisema Dkt. Mashinji.

Kwa upande wake Afisa Kilimo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emmanuel Mayyo alisema kuwa vipando bustani vya kisasa vina faida kubwa kwa walaji wa mboga za majani kwasababu wanaimarisha afya na kuondoa hatari ya magonjwa nyemelezi. Ni muhimu sana katika mlo wa kila siku kuwa na mboga za majani na matunda, wananchi waje wajielimishe ili wakapande mboga kwenye maeneo yao hata kwa udogo hivyo hivyo. Kila mboga ina faida zake mwilini kwa maana hiyo tukizingatia hilo tutatengeneza afya zetu muda wote na kuepuka maradhi nyemelezi yanayotakana na kukosa virutubisho muhimu mwilini” alisema Mayyo.

Alimalizia kwa kuwaalika wananchi wote kutembelea vipando bustani vya halmashauri ili kujifunza namna ya kupanda mboga mboga na matunda katika eneo dogo. “Nawakaribisha sana watu wote katika banda letu. Tuna teknolojia za kisasa ambazo zinawezesha hata mtu anayeishi nyumba ya kupanga kuwa na namna ya kupata mboga za majani muda wote. Kwasasa kwa ubunifu wa njia hizi nafuu, kukosa mboga za majani katika mlo ni mtu ajitakie mwenyewe” alimaliza Mayyo.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma lapewa angalizo lishe bora kwa wananchi

RC Dodoma apongeza wafugaji kwa ushiriki wa Paredi ya Mifugo

Rais Samia: Tumieni kikamilifu Miundombinu, Teknolojia na mitaji iliyowekezwa katika Kilimo, Uvuvi na Mifugo