Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu
Na. Coletha Charles, MATUMBULU Wananchi wa Mtaa wa Ukombozi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wameadhimisha Samia Day 2026 kwa kushiriki bonanza lililojumuisha michezo, burudani na shughuli za kijamii katika viwanja vya Shule ya Msingi Matumbulu. Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali kama salakasi, soka, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, bao, ngoma na kula, huku wananchi wakipata fursa ya kushiriki na kujumuika katika maadhimisho hayo. Akizungumza katika bonanza hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Matumbulu, Zuberi Mbawala alisema kuwa maandalizi hayo yalilenga kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika shughuli za pamoja huku wakipata elimu kuhusu afya na lishe. “Tumefanya michezo na shughuli mbalimbali za kijamii kwa lengo la kuwapa wananchi burudani, kuonesha vipaji na kuimarisha mshikamano. Lengo letu ni kuendelea kutoa hamasa, kuimarisha mshikamano na kuhakikisha jamii yetu inapata fursa ya kufurahia na kushiriki katika shughuli zenye manufaa,” ...