MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ZA ARDHI WACHANGIA ONGEZEKO LA WANAWAKE KUMILIKI ARDHI NCHINI

Na Eleuteri Mangi WANMM Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia umeongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi nchini kutoka asilimia 25 hadi 35 hatua inayosaidia kuinua kiuchumi wao na taifa kwa ujumla. Kauli hiyo imetolewa na Mratibu Mradi LTIP Bw. Joseph Shewiyo unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati akifungua kikao kazi cha Asasi za kiraia kujadili utekelezaji wa mradi huo Januari 16, 2024 jijini Dodoma. "Mna jukumu kubwa, mnapaswa kuongeza wigo katika kutekeleza majukumu yenu kufanikisha kutoa hati milki za kimila ili kuinua uchumi wa wananchi, mna mchango mkubwa kwa ongezeko la wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 25 hadi 35, mkafanye kazi yenu kwa weledi msiharibu ndoa za watu" amesema Bw. Shewiyo. Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Benki ya Dunia...