Dodoma Jiji FC yatangaza benchi la ufundi msimu wa 2025/2026
Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu
ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imemtambulisha Mashami Vicent raia wa Burundi kuwa
kocha wake mkuu kuelekea kwenye msimu wa mashindano ya ligi kuu ya NBC msimu wa
mwaka 2025/2026, sanjari na hilo imemtambulisha Bakira Guy raia wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kuwa kocha msaidizi wa klabu hiyo.
Hayo yalibainishwa na Novatus John, Mtendaji Mkuu wa Dodoma Jiji FC, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Vizano jijini Dodoma ukiwa na lengo la kutambulisha benchi jipya la ufundi.
“Baada
ya kuvunja benchi letu zima la ufundi tulilokuwa nalo msimu uliopita, kama
uongozi tulikaa chini na kuanza mchakato rasmi wa kutafuta benchi jipya la ufundi.
Tulikuwa makini kupitia “CV” za makocha mbalimbali hatimae tukaweza kupata
kocha bora zaidi ya wote na ndiye huyu ambaye tumemtangaza. Kwa upande wetu
tutampatia stahiki zake zote ili timu yetu ifanye vizuri zaidi msimu ujao”
alisema John.
Mashami
Vicent kabla ya kutuwa Dodoma Jiji FC, alikuwa akiiongoza klabu ya Polisi FC,
inayoshiriki ligi kuu nchini Burundi, akiisaidia timu hiyo kushinda makombe
manne na kufanikiwa kuipeleka klabu hiyo kwenye mashindano ya shirikisho barani
Afrika baada ya kupita miaka 10, pia amehudumu katika kikosi cha timu ya Taifa
ya Burundi “Amavubi’’ kwa muda wa miaka minne.
Kuelekea msimu ujao wa mashindano Dodoma Jiji FC, itakita kambi jijini Arusha kwaajili ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano wa Ligi kuu ya NBC Tanzania bara, kambi hiyo inatarajia kuwa ya wiki tatu kuanzia Agosti 10, huku kambi hiyo ikilenga kuhusisha michezo mbalimbali ya kirafiki kwaajili ya kutafuta muunganiko wa timu, alisema.
Katika
hatua nyingine Dodoma Jiji FC, inaendelea na zoezi la usajili ambapo mpaka sasa
imekwisha watambulisha wachezaji mawili ambao ni Miraji Abdallah na kiungo
Nelson Munganga. Alisema John.
Comments
Post a Comment