DC Shekimweri ashauri TMDA kuwa wabunifu
Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Mkuu
wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj. Jabir Shekimweri, ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa
Tiba (TMDA) kuwa wabunifu na kutumia teknolojia ya kisasa katika shughuli zake
za ukaguzi wa dawa na vifaa tiba nchini, ili kuongeza ufanisi na kuimarisha
usalama wa wananchi.
Alisema hayo wakati alipotembelea banda la TMDA katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Alisema
kuwa anawapongeza
kwa kuendelea kutoa huduma ikiwemo kusajili, kudhibiti na kufuatilia ubora wa
dawa. “Nawapongeza
kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kulinda afya za wananchi kupitia udhibiti wa dawa
na vifaa tiba. Hata hivyo, katika dunia ya sasa ya teknolojia, mnapaswa kuwa
wabunifu zaidi katika mbinu zenu za ukaguzi ili kuweza kufika maeneo mengi kwa
haraka na kwa ufanisi zaidi na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi
sahihi ya dawa” alisema Alhaj. Shekimweri.
Pia aliongezea kwa kuwasisitiza kuendelea kushirikiana kwa karibu na
vyombo vingine vya serikali. “Na niwaase tu Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba
kuendelea kushirikiana na baadhi ya taasisi nyingine ili kuwafikia wananchi
sehemu mbalimbali kwaajili ya kutoa elimu kuhusu matumizi ya dawa na
kuhakikisha kwamba bidhaa zote za afya zinazotumika nchini ni salama na zenye
ubora unaotakiwa” aliongeza
Alhaj.
Shekimweri.
Kwa
upande wake Mkaguzi wa Dawa Mwandamizi, Benedict Brashi alimshukuru Mkuu wa
Wilaya ya Dodoma kwa kutembelea banda lao na kuahidi kufanyia kazi yale ambayo
wameshauriwa. “Mamlaka hii inaendelea
kuboresha mifumo yake ya udhibiti na inaendelea kuwekeza kwenye teknolojia za
kisasa pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wake kwa lengo la kutoa huduma bora
zaidi kwa watanzania”
alisema Brashi.
Maonesho
ya Nanenane kitaifa yapo katika siku yake ya sita katika viwanja vya Nanenane,
Nzuguni yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Chagua viongozi bora kwa maendeleo ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi”
MWISHO
Imehaririwa na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment