Sura mpya ya kilimo cha vitunguu yaonesha mafanikio
Na. Husna Rajabu, DODOMA
Kitunguu kimekuwa ni miongoni mwa zao la biashara chenye
faida kubwa na hulimwa karibu maeneo yote nchini hasa maeneo ya miinuko ya
kaskazini mwa Tanzania.
Katika maonesho ya wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma vipando bustani vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma vimejumuisha teknolojia ya ulimaji vitunguu kwa njia ya asili katika eneo dogo na kupata mazao mengi.
Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Madei Kidai alieleza mchakato wa kilimo hicho chenye tija kibiashara. “Ili
kufanikisha kilimo cha vitunguu, ni lazima uanze na maandalizi ya shamba. Pia,
tunawahimiza wakulima kutafuta mbegu bora, kuandaa matuta vizuri, na kuhamisha
miche kutoka kwenye kitalu baada ya muda muafaka. Hapa kwetu tumetumia mbinu
hizi, na matokeo yanaonekana kama hivi mnavyoona” alieleza Kidai.
Kwa mujibu wa Kidai, baada ya kupanda, hatua
muhimu zinazofuata ni umwagiliaji na udhibiti wa wadudu na magonjwa. Alisisitiza
kuwa wametumia viwatilifu vinavyosaidia kudhibiti wadudu kama vidudu mafuta na
viducali na magonjwa kama fangasi ambayo kwa kawaida hushambulia vitunguu.
Kwa upande mwingine, Afisa Kilimo katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Nkunde Kimweri alieleza mbinu za kilimo hai ‘organic’
walizotumia. “Hapa katika shamba letu la mfano, tulianza kwa kuandaa matuta na
kuchanganya mbolea ya samadi. Kwa kila tuta tulitumia ndoo tatu za mbolea ya
samadi, baada ya kuchanganya mbolea na udongo, tulimwagilia maji na kuacha
ardhi ipoe kwa siku mbili kabla ya kupanda vitunguu” alisema Kimweri.
Alimalizia kusema kuwa mbegu wanazichagua kwa
umakini mkubwa sana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo. “Mbegu yetu, inaitwa
Red Planet F1, tuliipanda tarehe 20 Mei, 2025. Muhimu zaidi ni kwamba kilimo
hiki chote tumetumia mbolea na dawa za asili kama mnavyoona matokeo ni mazuri
na vitunguu vimestawi vizuri. Alimaliza Kimweri.
Vitunguu ni zao la kibiashara lenye tija
kubwa na linafanya vizuri mkoani Dodoma, linapaswa kupewa kipaumbele na
wakulima wengi kwa lengo la kukuza biashara ya vitunguu na kuongeza pato la
uchumi wa mkoa na wananchi wote kwa ujumla.
MWISHO
Imehaririwa na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment