Dodoma yaweka historia kwa utiaji saini mkataba wa huduma za ushauri elekezi kidigitali
Na. Coletha Charles, DODOMA
Halmshauri
ya Jiji la Dodoma na Kampuni ya Heerim Architects & Planners ya Korea Kusini
zimesaini mkataba wa upembuzi yakinifu na uandaaji wa Mpango Kabambe wa Mji wa
Kisasa wa Hombolo (HOTSAC).
Utiaji saini huo umefanyika Chinangali Park, Kata ya Chamwino, jijini Dodoma, kwa njia ya kidijitali, ukiashiria hatua mpya katika matumizi ya teknolojia kwenye shughuli za kiutawala na miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi
wa Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa utaratibu huo unaonesha
mabadiliko kutoka matumizi ya nyaraka za karatasi kwenda mifumo ya kidijitali,
kwa kuzingatia matakwa ya sheria kikamilifu.
Alisema
kuwa maandalizi ya mradi yalihusisha tafiti na ziara za mafunzo katika nchi
mbalimbali, zilizolenga kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kutoa ushauri na
kushiriki kikamilifu katika uandaaji wa mpango mpya.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Heerim Architects & Planners, Young Kyoon Jeong
alisema kuwa kampuni hiyo italeta utaalamu na uzoefu wa kimataifa katika
usanifu na upangaji wa mji wa kisasa na kidigitali duniani.
Jeong alisema kuwa Heerim itatumia uwezo wake wote wa kitaalamu kuandaa miundombinu inayokidhi viwango vya kimataifa, huku ikiheshimu urithi wa eneo husika na kuzingatia uhifadhi wa mazingira rafiki.
Nae,
Mratibu wa Mradi wa Mji wa Kisasa Hombolo, Azor William alisema kuwa eneo
linalopangwa kuendelezwa lina ukubwa wa hekta 24,000, likilenga kuunganisha Uwanja
wa Ndege wa Msalato, Mji wa Serikali na Bandari kavu kwa pamoja.
Alisema
kuwa eneo hilo limepangwa kuwa Smart City, lenye teknolojia za kisasa, mifumo
jumuishi ya usafiri, matumizi ya nishati mbadala na miundombinu inayozingatia
uhifadhi wa mazingira.
Aliongeza
kuwa utekelezaji utatumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP),
huku wawekezaji wakitarajiwa kuchangamkoa fursa katika utekelezaji wa mradi
huo.
Mkataba
huo umesainiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma pamoja na Mwanasheria wa Jiji la
Dodoma kwa upande wa serikali, huku Kampuni ya Heerim Architects & Planners
ikiwakilishwa na Mwenyekiti wake, Young Kyoon Jeong.
MWISHO


Comments
Post a Comment