Wazee Dodoma wataka Gereji kuondolewa katikati ya jiji
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Wazee na Wadau wa Maendeleo Dodoma wameitaka
Halmashauri ya Jiji kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya magereji na kuhamisha
shughuli hizo kutoka katikati ya jiji, wakisema hatua hiyo itapunguza
msongamano, kuimarisha usalama na kuboresha mandhari.
Wito huo umetolewa katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jiji la Dodoma, kilichoongozwa na Mstahiki Meya na kuwashirikisha wazee, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa
Umoja wa Gereji Tanzania, Richard Daud alisema kuwa kuendelea kuwepo kwa gereji
katika maeneo ya makazi na katikati ya jiji kunaweza kuhatarisha usalama wa
wananchi, kuongeza msongamano na kuchangia uchafuzi wa mazingira.
Alisema kuwa ni muhimu Jiji kutenga maeneo maalumu
yatakayokusanya pamoja magereji na biashara zinazohusiana na huduma za magari,
ili wafanyabiashara wapate maeneo rasmi ya kuendeshea shughuli zao.
“Gereji zimesongamana mjini kiasi ambacho haifai kabisa. Kila mahali mtu anafungua gereji. Tunamuomba Meya aondoe magereji yote hapo mjini, kusiwe na magereji. Wananchi wawe wanakuja kupata huduma za magari nje ya mji, jambo ambalo litasaidia kupanga matumizi ya ardhi ndani ya jiji,” alisema Daudi.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma,
Alimwoni Chaula, alisema kuwa kikao hicho kililenga kupata maoni ya wazee na
wafanyabiashara kuhusu mambo ambayo Jiji linaweza kuyaboresha ili kurahisisha
maisha ya wakazi.
Alisema kuwa wazee wamepewa nafasi ya kwanza kutokana
na uzoefu wao wa muda mrefu wa kuishi Dodoma, huku baadhi yao wakiwa wameishi
jijini humo kwa zaidi ya miaka 40 na 50.
“Tunataka tupate uzoefu kwanza ya wale watu waliokaa
Dodoma na wanaoijua Dodoma yao, ili sasa mbeleni ukija kukaa na vijana au kundi
la watu wa kati, unakuwa umejua kutoka kwenye experience ya wazee,” alisema
Chaula.
Nae, Mjumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Dodoma, Faustin Makalinga alisema kuwa kikao kilichoongozwa na Meya wa Jiji la Dodoma, kimekuwa na mafanikio makubwa baada ya washiriki kutoa mawazo na mapendekezo ya namna ya kuendeleza jiji hilo.
“Kikao kimekuwa na mafanikio mazuri sana kwa sababu
watu wametoa michango ya kujenga, hasa kwa kuwa watendaji wa Serikali
walikuwepo. Tunaamini maoni na mawazo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi na
Ofisi ya Jiji la Dodoma chini ya uongozi wa Mstahiki Meya,” alisema Mwakalinga.
MWISHO
Comments
Post a Comment