CHMT Jiji la Dodoma yakutana na waganga wafawidhi wa vituo vya afya vya serikali na binafsi kujadili utekelezaji Bima ya Afya kwa Wote
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Kamati ya Afya ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma (CHMT) imekutana na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi pamoja na makatibu wa afya wa Jiji la Dodoma, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Sebastiani Pima alisema kuwa Tanzania imeanza kutekeleza mpango huo kwa awamu. Awamu ya kwanza ilihusisha usajili wa kaya zisizo na uwezo na makundi maalumu, huku awamu ya pili ikijumuisha usajili wa kaya hizo pamoja na wananchi wengine kupitia vifurushi mbalimbali ya bima ya afya.
Dkt. Pima alisema kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kupitia bima katika vituo vya serikali na binafsi, akisisitiza kuwa hakuna mwananchi anayepaswa kuachwa nyuma. Aliongeza kuwa kikao hicho kinalenga kutoa elimu kuhusu mifumo ya utekelezaji, taratibu za usajili wa wanachama na namna ya kuwahudumia wanapofika katika vituo vya afya.
Aidha, aliwataka watoa huduma, hususan vituo binafsi, kutumia kikao hicho kuuliza maswali na kutoa maoni kuhusu changamoto za utekelezaji, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali, ili kuhakikisha mwanachama mwenye bima hapati vikwazo anapohitaji huduma za afya.
Vilevile, Dkt. Pima aliwataka waganga wafawidhi na watumishi wa vituo vya afya kuwa mabalozi wa mpango huo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya, namna ya kujisajili mtandaoni na kuwasaidia pale wanapohitaji msaada wa usajili, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila wananchi kuwa na afya bora.
Akizungumza kwa niaba ya waganga wafawidhi, Dkt. Ngoyeji Nkinga, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kiwanja cha Ndege, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vituo vya serikali na binafsi katika kufanikisha mpango huo, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma kwa wakati na kwa utaratibu unaotakiwa.






Comments
Post a Comment