Diwani Iyumbu apongezwa usimamizi miradi
Na. Dennis Gondwe, IYUMBU
DIWANI wa Kata ya Iyumbu amepongezwa kwa kusimamia
miradi ya maendeleo na kutakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wataalam wa
kata hiyo ili kukamilisha miradi kwa wakati ili iweze kutoa huduma kwa
wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipoongoza Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji kutembelea na kukagua ukamilishaji wa madarasa mawili, maabara tatu, jengo la utawala na matundu nane ya vyoo katika Shule ya Sekondari Iyumbu.
“Mheshimiwa Diwani ninakupongeza kwa kusimamia vizuri
miradi katika Kata ya Iyumbu. Kwa umoja huu kata inakwenda kubadilika
kimaendeleo, wape ushirikiano wataalam katika kata ili kuharakisha utekelezaji
wa miradi ya maendeleo. Kwa nafasi yako upo katika wakati mzuri zaidi
kuhamasisha wananchi kujitolea kushiriki shughuli za maendeleo na nguvu kazi”
alisema Dkt. Sagamiko.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Iyumbu, Sadick
Mpondamali aliishukuru halmashauri kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na kuahidi kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo.
Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Vincent Odero alisema kuwa kwa mujibu wa mpango kazi wa
utekelezaji wa mradi, vifaa vinatakiwa kuwa eneo la mradi angalau siku saba
kabla ya kazi husika ili kutokusababisha mkwamo wa kazi.
Awali akiikaribisha Timu ya Menejimenti ya Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Mwl. Fredrick Mwakisambwe
aliwataarifu kuwa shule hiyo ilipokea shilingi 168,000,000 kwa ajili ya
ukamilishaji wa madarasa mawili, maabara tatu, matundu nane ya vyoo na jengo la
utawala fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.
MWISHO
Comments
Post a Comment