Lishe bora yajengewa hamasa kupitia Samia Day Kata ya Uhuru
Na. Rahma Magona, UHURU
Elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora imetolewa katika
Kata ya Uhuru jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Samia
yaliyofanyika katika Uwanja wa Mtekelezo, ambapo wananchi na vijana
walielimishwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia mlo kamili.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Uhuru, Saada Zahaze alisema kuwa lishe bora imegawanyika katika makundi matano ambayo ni nafaka na vyakula vya wanga, matunda, mafuta, mbogamboga pamoja na vimiminika kama maji.
Aliongeza kuwa katika zoezi hilo wananchi walipatiwa
elimu kwa vitendo juu ya kupika uji uliowekwa ‘Blue Band’ kama chanzo cha
mafuta, pamoja na matunda mbalimbali ikiwemo matikiti na maembe, huku
mbogamboga kama mchicha zikitumika kuonesha umuhimu wa makundi hayo katika mlo
wa kila siku.
Zahaze alisisitiza kuwa Uwanja wa Mtekelezo
umechaguliwa kwa kuwa ni eneo kubwa linalokusanya watu wengi huku Kata ya Uhuru
ikiwa ni eneo la kibiashara hivyo shughuli hiyo imekuwa fursa ya kuwafikia
wananchi wengi kwa urahisi kupitia michezo na shughuli mbalimbali.
Vijana walioshiriki katika mchezo wa mpira wa miguu walipatiwa elimu kuhusu lishe bora huku wakisisitizwa kuwa vijana ni sehemu muhimu ya taifa na elimu hiyo inaweza kuwasaidia kuzingatia lishe bora katika maisha yao na familia zao.
MWISHO
Comments
Post a Comment