Dodoma yaweka mikakati ya kuimarisha usafi wa Mazingira
Na. Mwandishi wetu, MSALATO
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweka mikakati
mbalimbali ya kuimarisha usafi wa mazingira kwa kuongeza usimamizi katika ngazi
za kata na mitaa, kuimarisha mfumo wa uondoshaji taka na kuongeza ushiriki wa
wananchi na sekta binafsi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mikakati hiyo katika
Kata ya Msalato, Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka Ngumu wa jiji
hilo, Mkana Mkana alisema kuwa halmashauri inalenga kuhakikisha usafi wa
mazingira unakuwa sehemu ya utamaduni wa kila siku.
Alisema kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni kuunda
Kamati za Usafi wa Mazingira katika ngazi za kata na mitaa, ambazo zitasaidia
kufuatilia hali ya usafi na kuongeza uwajibikaji katika maeneo yanayowazunguka
wananchi.
“Tutaanzisha mashindano ya usafi katika mitaa na kata
kila robo mwaka ili kuongeza hamasa ya wananchi, huku tukichukua hatua dhidi ya
kampuni na vikundi vya uondoshaji taka vitakavyoshindwa kutekeleza wajibu wao,”
alisema Mkana.
Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kutangaza zabuni
za usafishaji, ukusanyaji na usafirishaji wa taka katika kata na mitaa ambayo
bado haina wazabuni wa kutosha, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa uondoshaji
taka.
Katika hatua nyingine, Mkana alisema kuwa mafanikio
yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli hizo yamechangiwa na muitikio
chanya wa jamii, hali ambayo imeongeza kiwango cha usafi wa mazingira katika mitaa
na kata mbalimbali.
Aidha, ushirikiano na uratibu wa pamoja kati ya
makundi mbalimbali ya watendaji na sekta binafsi umeongezeka, jambo ambalo
limewezesha shughuli za usafi wa mazingira kutekelezwa kwa ushirikiano zaidi.
Katika kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma yaliyotolewa tarehe 4 Septemba,
2026, halmashauri itaendelea kudumisha mazingira safi, salama na yenye afya
kupitia ushiriki endelevu wa jamii katika usafi na udhibiti wa taka ngumu.
MWISHO
Comments
Post a Comment