Dawati la Jinsia Jiji la Dodoma lafikia watu 2,133

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Dawati la Jinsia na Watoto Jiji la Dodoma limewafikia watu 2,133 kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuhamasisha malezi bora ya watoto katika Mwezi wa Maendeleo ya Jamii.

 


Akitoa taarifa hiyo, Mratibu wa Jinsia na Watoto Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fatuma Daudi alisema kuwa wanawake 1,376 na wanaume 757 walipewa elimu kupitia mikutano ya jamii na shughuli za uhamasishaji zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji.

 

Alisema kuwa elimu hiyo iliwafikia wazazi na walezi pamoja na makundi mbalimbali ya jamii, yakiwemo madereva wa bodaboda katika Kata za Chigongwe na Makole, huku wananchi wa Kata za Chihanga, Chang’ombe, Ihumwa, Madukani na Ngh’ong’ohna nao wakipatiwa elimu hiyo.

 

“Katika Mwezi wa Maendeleo ya Jamii, tumewafikia watu 2,133, wakiwemo wanawake 1,376 na wanaume 757, kwa kuwapatia elimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia na umuhimu wa malezi bora kwa watoto,” alisema Daudi.

 

Kwa upande wa vijana, alisema kuwa elimu ilitolewa kwa vijana balehe katika Kata za Mbabala na Matumbulu, huku wanafunzi katika Shule za Sekondari Makole, Sechelela na Miyuji pamoja na Shule ya Msingi Ngh’ong’ohna nao walifikiwa.

 

Aidha, Daudi alisema kuwa sambamba na utoaji wa elimu kwa jamii, wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya halmashauri walipatiwa mafunzo kutoka kwa wataalamu wa mkoa kwa kushirikiana na wadau wa SOS.

 

“Mafunzo haya yalilenga kuwawezesha wajumbe wa kamati kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili katika jamii, kwa kuwaongezea uelewa na uwezo wa kutambua, kuzuia na kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo hivyo,” alisema Daudi.

 

Dawati liliendelea kuratibu shughuli za Ulinzi na Usalama wa Mtoto ndani na nje ya shule kwa kushirikiana na Divisheni za Elimu ya Msingi na Sekondari, ikiwamo kutembelea Shule ya Msingi Generali Msuguli kukagua utekelezaji wa majukumu hayo kwa kushirikiana na walimu wa malezi.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Polisi Kata waungana zoezi la Usafi wa Mazingira Dodoma

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 14.7 Maadhimisho ya Samia Day

Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu