Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 14.7 Maadhimisho ya Samia Day
Na. Coletha Charles, MATUMBULU
Kata ya Matumbulu imepokea mikopo ya asilimia 10 yenye
thamani ya shilingi milioni 14.785 kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu, ikiibua fursa za kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika maadhimisho ya Samia Day, 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Matumbulu, Mtaa wa Ukombozi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata hiyo, Merina Gombo alisema kuwa mikopo hiyo imewanufaisha wananchi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Alisema kuwa walengwa wa mikopo hiyo ni wanawake,
vijana na watu wenye ulemavu, ambao wamepata fursa ya kuendesha shughuli
mbalimbali za kiuchumi na kujiongezea kipato.
“Wananchi na jamii ya Matumbulu wamenufaika sana na
wamepata maendeleo kupitia mikopo hiyo. Hadi sasa, Kata ya Matumbulu imepokea
shilingi milioni 14.785 kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi
maalum,” alisema Gombo.
Kwa upande wake, mkazi wa Mtaa wa Muungano, Kata ya
Matumbulu, Suzana Albert alisema kuwa vijana wamekuwa miongoni mwa wanufaika wa
mikopo hiyo, inayowasaidia kujitegemea na kujikwamua kiuchumi.
“Mkopo huu umetusaidia vijana kuimarisha shughuli zetu
za kiuchumi na kujitegemea. Tunashukuru serikali kwa kutuwezesha kupitia mikopo
hii, ambayo imekuwa chachu ya kuinua hali yetu ya kiuchumi,” alisema Albert.
Maadhimisho ya Samia Day 2026 katika Kata ya Matumbulu
yaliambatana na bonanza kubwa lililoshirikisha michezo mbalimbali, likiwamo
soka, ngoma na mchezo wa kukimbiza kuku pamoja na mambo mengine.
MWISHO
Comments
Post a Comment