Polisi Kata ya Uhuru atoa elimu ya usafi wa Mazingira
Na. Rahma Magona, UHURU
Wananchi wa Kata ya Uhuru Halmashauri ya Jiji la
Dodoma wameshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Samia yaliyofanyika katika
Uwanja wa Mtekelezo, ambapo walifanya usafi wa mazingira, kushiriki michezo pamoja
na kupata elimu kuhusu lishe na usalama.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Inspekta Haruna Ngereza, Polisi Kata ya Uhuru, alisema kuwa wananchi walishiriki katika zoezi la usafi wa mazingira, kabla ya kuendelea na mchezo wa mpira wa miguu na kupatiwa elimu kuhusu lishe pamoja na virutubisho vya lishe.
Inspekta Ngereza aliongeza kuwa wananchi walipatiwa
elimu kuhusu usalimishaji wa silaha zinazomilikiwa kinyume na sheria huku
akiwataka wenye silaha hizo kuzisalimisha katika kituo cha Polisi, Ofisi ya Afisa
Mtendaji wa kata au Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Mtaa husika ili taratibu za
kisheria ziweze kufuatwa na wahusika kunufaika na msamaha uliopo.
Aidha, alisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni zoezi
endelevu linalopaswa kufanyika kila siku na si kusubiri siku maalumu, akiwataka
wananchi kuendelea kuzingatia usafi katika maeneo yao kwa kuunga mkono wito wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Sambamba na hilo alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwa kusisitiza umuhimu wa kuifanya Dodoma kuwa jiji la kijani huku akisema Kata ya Uhuru inaendelea na zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Uhuru.
MWISHO
Comments
Post a Comment