Samia Day Kata ya Uhuru yatoa hamasa ya ujio wa AFCON, 2027

Na. Rahma Magona, UHURU

 

Maadhimisho ya Siku ya Samia yamefanyika katika Kata ya Uhuru jijini Dodoma kwa lengo la kutoa hamasa kwa wananchi kuhusu ujio wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yanayotarajiwa kuanza Juni mwakani, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli mbalimbali.

 


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Mtendaji Kata wa Kata ya Uhuru, Denis Katunzi alisema  kuwa shughuli hizo zilianza kwa kutoa elimu kwa mama lishe kuhusu matumizi ya nishati safi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira na kuachana na matumizi ya mkaa.

 

Katunzi alisema kuwa maadhimisho hayo yaliendelea kwa zoezi la upandaji miti ya matunda katika Shule ya Msingi Uhuru, kabla ya wananchi kushiriki katika usafi wa mazingira kuzunguka uwanja, huku akisema shughuli hizo zililenga kuimarisha utunzaji wa mazingira na afya za wananchi.

 

Aliongeza kuwa siku hiyo pia ilihusisha mchezo wa mpira wa miguu kati ya Timu ya Kipande FC na KBC FC, ambapo Timu ya mpira KBC iliibuka mshindi na kukabidhiwa zawadi ya mbuzi mnyama, huku elimu ya lishe kuhusu umuhimu wa mlo kamili ilitolewa hasa kwa wa kina mama na watoto.

 


Afisa Mtendaji huyo aliwashukuru mamia ya wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika maadhimisho hayo, akisema ushiriki wao umewezesha ujumbe kuhusu matumizi ya nishati safi, lishe, utunzaji wa mazingira na hamasa ya ujio wa AFCON 2027 kuwafikia.

Comments

Popular Posts

Polisi Kata waungana zoezi la Usafi wa Mazingira Dodoma

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 14.7 Maadhimisho ya Samia Day

Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu