Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu

Na. Coletha Charles, MATUMBULU

 

Wananchi wa Mtaa wa Ukombozi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wameadhimisha Samia Day 2026 kwa kushiriki bonanza lililojumuisha michezo, burudani na shughuli za kijamii katika viwanja vya Shule ya Msingi Matumbulu.

 


Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali kama salakasi, soka, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, bao, ngoma na kula, huku wananchi wakipata fursa ya kushiriki na kujumuika katika maadhimisho hayo.

 

Akizungumza katika bonanza hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Matumbulu, Zuberi Mbawala alisema kuwa maandalizi hayo yalilenga kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika shughuli za pamoja huku wakipata elimu kuhusu afya na lishe.

 

“Tumefanya michezo na shughuli mbalimbali za kijamii kwa lengo la kuwapa wananchi burudani, kuonesha vipaji na kuimarisha mshikamano. Lengo letu ni kuendelea kutoa hamasa, kuimarisha mshikamano na kuhakikisha jamii yetu inapata fursa ya kufurahia na kushiriki katika shughuli zenye manufaa,” alisema Mbawala.

 


Kwa upande wake, mkazi wa Mtaa wa Kaunda na mshindi wa mchezo wa kukimbiza kuku, Felister Frank alishauri kuwa maadhimisho ya Samia Day yawe yanaandaliwa kila mwezi ili wananchi wapate fursa ya kushiriki shughuli za michezo na kujumuika zaidi.

 

“Nimefurahi sana kupata ushindi huu wa kukimbiza kuku. Nawaomba waandaaji waendelee na Samia Day kila mwezi, kwa sababu inatupa nafasi ya kushiriki michezo, kujiburudisha na kujenga umoja miongoni mwa wananchi,” alisema Frank.

 

Nae, Mchezaji wa Mpira wa Timu ya Ipondela FC na washindi wa mpira wa miguu, Lucas Baraka alisema kuwa ushindi huo umeongeza ari kwa timu hiyo kuendelea kujifua na kutafuta fursa zaidi za kushindana.

 

“Haya mabonanza ni mazuri, na pia tunafurahia kwa ushindi mkubwa tulioupata kwa sababu wachezaji ilikuwa papatu papatu za kutosha, lakini Mungu ametujalia ushindi umekuwa kwetu,” alisema Baraka.

 


Bonanza hilo liliongozwa na kaulimbiu isemayo “Samia Day 2026, AFCON inakuja” liliwakutanisha wananchi katika mashindano, burudani na shughuli za kijamii, sambamba na elimu ya lishe, likitoa fursa ya kujenga mshikamano na kukuza vipaji.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Polisi Kata waungana zoezi la Usafi wa Mazingira Dodoma

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 14.7 Maadhimisho ya Samia Day