Waziri wa Ulinzi na JKT akutana na vijana walioshiriki ujenzi wa Ikulu ya Chamwino

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walioshiriki katika ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.

 


Mazungumzo hayo yalilenga kuwasikiliza vijana hao, kuwapongeza na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kutekeleza ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, ambayo ni moja ya alama muhimu za Taifa na Ofisi ya Juu katika mfumo wa Utawala na Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na vijana hao, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dkt. Rhimo Nyansaho alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua na kuthamini mchango, uzalendo na kujituma kwa vijana hao katika utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria.

Dkt. Nyansaho alisema kuwa serikali inatambua uvumilivu, nidhamu na kujitolea kwa vijana hao, ambao walishiriki katika kazi kubwa ya ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, na kwamba kukutana nao ni sehemu ya kuwapa shukrani na pongezi kwa mchango wao kwa Taifa.

 


“Serikali inatambua na kuthamini mchango wenu katika ujenzi wa mradi huu wa kihistoria. Mmetoa mchango mkubwa kwa Taifa na mmeonesha uzalendo, nidhamu na kujituma katika kutekeleza jukumu hili muhimu,” amesema Dkt. Nyansaho.

 

Kwa upande wao, wawakilishi wa vijana walioshiriki katika ujenzi wa Ikulu ya Chamwino wamemshukuru Waziri wa Ulinzi na JKT kwa uamuzi wa kukutana nao na kusikiliza maoni yao. Wamesema hatua hiyo imewapa faraja na kuonesha namna Serikali inavyotambua na kuthamini mchango wao katika ujenzi wa Taifa.

Aidha, vijana hao wamemwahidi Waziri wa Ulinzi na JKT pamoja na Serikali kwa ujumla kuwa wataendelea kudumisha uzalendo, uadilifu, nidhamu na kujitolea katika kulitumikia Taifa kwa nguvu zao zote, kama walivyofanya katika utekelezaji wa jukumu la ujenzi wa Ikulu ya Chamwino.

 



Mazungumzo hayo yalilenga kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha ustawi wa vijana waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na kutathmini namna bora ya kuwawezesha vijana hao kutumia ujuzi, nidhamu na uzoefu walioupata katika JKT kwa manufaa yao na maendeleo ya Taifa.

 

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe; Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele; pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

 

Comments

Popular Posts

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha taarifa ya ufungaji hesabu 2025/2026

Wilaya ya Dodoma kuchanja watoto zaidi ya laki 2 chanjo ya Polio