Wazazi wahimizwa kufuatilia elimu na tabia za watoto nyumbani

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Wazazi wamehimizwa kuwa na ushirikiano wa karibu na walimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao wanapokuwa nyumbani, ili kusaidia kukuza uwezo wao kitaaluma na kujenga msingi bora wa elimu, badala ya kutegemea walimu pekee katika jukumu hilo.



 

Wito huo ulitolewa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Shekinah Pre & Primary School, Obadia Mwambapa wakati wa siku maalumu ya kufunga shule, ambapo alisema kuwa ushirikiano kati ya wazazi na walimu ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na elimu bora. 

 

Alisema kuwa wazazi wanapaswa kutenga muda wa kufuatilia masomo ya watoto wao, kujua changamoto wanazokutana nazo na kushirikiana na walimu katika kutafuta suluhisho.

 

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Juliana Sabrere alisema kuwa ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu la pamoja kati ya walimu na wazazi, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kulinda maadili mema ya watoto na kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yenye malezi yanayozingatia misingi ya heshima, uwajibikaji na nidhamu.



Alisema kuwa malezi bora ya watoto yanahitaji ushiriki wa pande zote mbili, kwa kuwa mtoto anahitaji uangalizi na mwongozo akiwa shuleni na nyumbani.


Aidha, aliwataka wazazi na walimu kuwa karibu na watoto, kuwasikiliza na kuwasaidia kutambua mambo mema na mabaya ili kujenga kizazi bora cha sasa na cha baadaye.



Comments

Popular Posts

Wafanyabiashara Soko la Miembeni Waazimia Kulinda Usafi

Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha taarifa ya ufungaji hesabu 2025/2026

Wilaya ya Dodoma kuchanja watoto zaidi ya laki 2 chanjo ya Polio