Serikali yafikisha Umeme katika maeneo 582 ya wachimbaji wadogo, kilimo na viwanda Tanzania bara
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Naibu Waziri wa
Nishati, Salome Makamba, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) imetekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme katika maeneo 582 ya wachimbaji
wadogo, kilimo na viwanda Tanzania Bara, kwa gharama ya shilingi bilioni 115.
Makamba aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mwanahamisi Athumani, Mbunge wa Viti Maalumu, aliyetaka kujua ni lini serikali itatekeleza Mpango Mkakati Maalumu wa kuhakikisha maeneo ya wachimbaji wadogo yanafikishiwa umeme wa kutosha kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.
Akijibu swali hilo,
Makamba alisema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili, 2023 na kwa sasa
umefikia hatua za mwisho za utekelezaji.
Aidha, alisema kuwa
Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaendelea kuainisha
maeneo ya kipaumbele yatakayofikishiwa huduma ya umeme katika hatua
zinazofuata, kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
Sambamba na hilo, alisema
kuwa serikali kupitia TANESCO, kwa kutumia fedha za ndani, inaendelea
kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa
umeme pamoja na ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kupoza umeme katika mikoa
mbalimbali nchini, hususan maeneo yenye changamoto ya low voltage.
Alisema kuwa hatua
hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji
yanafikiwa na huduma ya umeme ya kutosha na ya uhakika.
Makamba alisisitza kuwa
lengo la serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo, wakulima, viwanda na maeneo
mengine ya uzalishaji yanapata umeme wa kutosha na wa uhakika wakati wote, ili
kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa shughuli
za kiuchumi nchini.
Comments
Post a Comment