Wananchi watakiwa kuunga mkono juhudi za usafi wa Mazingira

Na. Ramadhani Mohammed, MIYUJI

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtamaa, Kata ya Miyuji mkoani Dodoma, Hapines Joshua amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kudumisha usafi wa mazingira ili kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi na salama kwa afya za wakazi wake.



Akizungumza wakati wa zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika Jumamosi, amesema kuwa ushirikiano kati ya wananchi na serikali ni muhimu katika kufanikisha juhudi za kuboresha usafi wa mazingira, huku akieleza kuwa shughuli hizo zinaendelea kufanyika kila siku katika maeneo mbalimbali, ikiwemo nyumba kwa nyumba.

“Wito wangu kwa wananchi, naomba tuendelee kujiandaa na mvua hizi za El Niño na kutunza mazingira kwa sababu kama tunavyojua, mazingira yakiwa machafu kipindi cha mvua kama hizi kunaweza kuwa na milipuko ya magonjwa mbalimbali kama kipindupindu na magonjwa ya tumbo. Kwa hiyo, hamasa yangu ni tuendelee kushirikiana kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa safi,” amesema Joshua

Kwa upande wake, mwananchi wa Kata ya Miyji, Kelvin Nyange amesema kuwa wananchi wako tayari kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha usafi wa mazingira unakuwa wa kiwango cha juu na kulifanya Jiji la Dodoma kuwa mfano wa usafi nchini.

“Sisi, wananchi tuko mkono kwa mkono na Serikali yetu kuhakikisha usafi unazidi kuwa wa hali ya juu na Jiji la Dodoma liwe la mfano kwa usafi nchini,” amesema Nyange.



Aidha, amewahimiza wananchi kuendeleza utamaduni wa kufanya usafi katika maeneo yao ya makazi na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zinazolenga kuboresha mazingira, akieleza kuwa jukumu la usafi linahitaji ushiriki wa kila mmoja.

Zoezi hilo la usafi wa mazingira ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kuimarisha usafi na kujiandaa na msimu wa mvua, kwa lengo la kupunguza hatari ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na mazingira machafu na kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi wakati wote.

Comments

Popular Posts

Wananchi watakiwa kuzingatia taratibu za kupata Hati ya kusafiria Dodoma

Vikundi vya Kata ya Kizota vyapatiwa elimu ya mikopo ya 10%

Watumishi watakiwa kuzingatia nidhamu na mshikamano kazini