Vikundi vya Kata ya Kizota vyapatiwa elimu ya mikopo ya 10%
Na. Mwandishi wetu, KIZOTA
Vikundi
vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Kata ya Kizota vimepatiwa
elimu kuhusu taratibu za kuomba mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa robo ya pili ya mwaka, inayotarajiwa kutolewa katika kipindi cha mwezi
Oktoba, 2026.
Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Lechasa, Kata ya Kizota, ikiwa na lengo la kuviandaa vikundi hivyo kuelewa taratibu na masharti ya mikopo hiyo ili viweze kunufaika na fursa zinazotolewa na halmashauri.
Akizungumza
katika semina hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kizota, Ilumva Hoka
amevihimiza vikundi kuendelea kujiandaa na kujisajili kwa mujibu wa taratibu
zilizowekwa ili viweze kutumia fursa hiyo kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Amesema
kuwa katika kipindi hiki cha mwezi Oktoba, 2026 kiasi cha shilingi bilioni 7.5
kinatarajiwa kutolewa kwa ajili ya mikopo hiyo, huku katika Kata ya Kizota
zaidi ya vikundi vitano vikitarajia kuwasilisha maombi ya mikopo.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Vijana cha Makaniki Group, George Mapunda amesema kuwa kikundi chao kimejiandaa kunufaika na fursa hiyo, huku akiwahimiza vijana wengine kujitokeza na kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi.
Mapunda
amewataka vijana kufika katika ofisi za watendaji wa maeneo yao ili kupata
maelekezo na kufahamu taratibu zinazopaswa kufuatwa katika kuanzisha, kusajili
na kuwasilisha maombi ya mikopo hiyo.
Amesisitiza
kuwa ushiriki wa vijana katika fursa hizo ni muhimu katika kukuza shughuli za
ujasiriamali, kuongeza kipato na kuimarisha uwezo wao wa kujitegemea kiuchumi.
Vikundi vimeaswa kuzingatia masharti na taratibu za mikopo hiyo, pamoja na kuhakikisha vinakuwa na mipango madhubuti ya matumizi ya fedha ili mikopo hiyo iweze kutoa matokeo chanya katika shughuli zao za maendeleo.


Comments
Post a Comment