Serikali yaweka Mkakati wa kukabiliana na madhara ya El Nino
Na. Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
SERIKALI imeandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño, huku ikikadiria kuwa inahitaji takribani Shilingi bilioni 730 kutekeleza hatua mbalimbali za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa katika msimu wa Vuli 2026/27.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi alisema kuwa serikali imeandaa mpango huo kwa lengo la kuimarisha utayari na kuchukua hatua za mapema katika kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya madhara yanayoweza kusababishwa na El Niño.
Alisema kuwa mpango
huo umeandaliwa kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) Agosti 18, 2026, uliotabiri uwepo wa hali ya El Niño yenye nguvu katika
msimu wa Vuli 2026/27.
Kwa mujibu wa Prof.
Kabudi, miongoni mwa hatua zilizopangwa na Serikali ni kukarabati na kuboresha
miundombinu ya barabara, madaraja, mitaro na reli, pamoja na kuimarisha huduma
muhimu za afya, elimu, maji, umeme na mawasiliano katika maeneo yanayoweza
kuathiriwa.
Alisema kuwa serikali
pia imepanga kuimarisha akiba ya chakula, vifaa vya uokoaji na misaada ya
kibinadamu, sambamba na kuandaa maeneo ya makazi ya muda kwa wananchi
watakaoweza kuathiriwa na maafa.
Hata hivyo, Prof.
Kabudi alisema kuwa makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutekeleza mpango
huo katika sekta zote ni takribani shilingi bilioni 730, wakati fedha
zilizotengwa katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 kwa shughuli
hizo kwa sekta zote ni shilingi bilioni 10.
Alisema kuwa tofauti
hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha maandalizi, uratibu na matumizi
bora ya rasilimali zilizopo ili kuhakikisha madhara yanayoweza kusababishwa na
mvua hizo yanadhibitiwa kwa wakati.
Prof. Kabudi aliwataka
wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na
kuchukua tahadhari mapema, ikiwemo kuondoka katika maeneo hatarishi yanayoweza
kukumbwa na mafuriko au maporomoko ya ardhi.
Aidha, wananchi walitakiwa
kuwa na akiba ya chakula na kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika endapo
maafa yatatokea.
Pamoja na tahadhari
hizo, Prof. Kabudi amesema Serikali inawahimiza wananchi kutumia fursa ya mvua
zinazotarajiwa kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa
maji na uvuvi.
Alisema kuwa wakulima
wanapaswa kutumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu
zinazofaa kwa msimu wa Vuli ili kunufaika na mvua hizo bila kuathiriwa na
madhara yanayoweza kujitokeza.
Alieleza kuwa Ofisi
ya Waziri Mkuu, Agosti 26, 2026, iliwaelekeza Wakuu wa Mikoa inayoweza
kuathiriwa na mvua za El Niño kuchukua hatua za maandalizi na kukabiliana na
madhara yanayoweza kujitokeza.
Prof. Kabudi alisisitiza
kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema, kufuatilia taarifa rasmi za
TMA na kuepuka maeneo hatarishi, huku wakitumia mvua hizo kama fursa ya
kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali.
Comments
Post a Comment