Watumishi wa Elimu watakiwa kuongeza tija kazini
Na. Mwandishi wetu,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.
Carolyne Nombo, amewapongeza watumishi wa wizara hiyo kwa kazi kubwa na
mafanikio waliyoyapata katika mwaka wa fedha uliopita, huku akiwataka kuendelea
kuyasema kwa ujasiri mafanikio hayo yaliyoiwezesha sekta ya elimu kung’aa
kitaifa na kimataifa.
Prof. Nombo alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na uongozi imara wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, na Naibu Waziri, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, pamoja na ushirikiano wa Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na watumishi wote.
Prof. Nombo alisema hayo jijini Dodoma wakati alipoongoza kikao
cha tafakuri cha uongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
kilicholenga kutathmini utekelezaji wa majukumu yaliyokabidhiwa kwa wizara. Aliwashukuru
watumishi kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao na kusisitiza umuhimu wa
kuendeleza ushirikiano katika kufikia malengo ya wizara.
Aidha, Prof. Nombo alisema kuwa mabadiliko makubwa yanayoendelea
katika sekta ya elimu yanatokana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu, ambayo
inalenga kuandaa wahitimu wenye ujuzi, kuboresha matokeo ya kujifunza na
kuimarisha mfumo mzima wa elimu nchini. Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya
Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza kwa kiwango
kikubwa katika sekta ya elimu kupitia ujenzi wa miundombinu, ajira za walimu,
mafunzo ya watumishi na fursa mbalimbali za kitaaluma.
Katika kikao hicho, Katibu Mkuu alikumbusha wajibu mkubwa wa
Wizara katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa
takribani asilimia 40 ya masuala yaliyomo kwenye dira hiyo yanahusu sekta ya
elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu. Ameongeza kuwa utekelezaji wa elimu ya
lazima kwa miaka 10 na maandalizi ya kupokea kundi la wanafunzi la double
cohort mwaka 2028 ni miongoni mwa majukumu makubwa yanayohitaji maandalizi ya
mapema na ushirikiano wa pamoja.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, aliwataka watumishi kuendelea kufanya kazi
kwa ushirikiano, weledi, nidhamu na uadilifu, akisema misingi hiyo ni muhimu
katika kuimarisha utendaji kazini.
Alisema kuwa mafanikio ya wizara yanatokana na mchango wa kila
mtumishi, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza ubunifu katika utendaji huku sheria,
kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma ikizingatiwa. Pia amesisitiza
umuhimu wa kuzingatia usalama wa taarifa za serikali na kuhakikisha wananchi
wanahudumiwa kwa furaha, ufanisi na weledi, huku akiwataka watumishi kutumia
mafunzo waliyopata kuongeza tija na kuhamasisha utamaduni wa kuendelea
kujifunza katika kila ngazi ya utumishi.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu katika
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Edith Rwiza, alisema kuwa kikao
cha uongozi na watumishi kimetoa fursa ya kutafakari kwa pamoja, kujenga
mshikamano na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.
Alisema kuwa kikao hicho pia kililenga kutafakari mafanikio, changamoto
na mafunzo yaliyopatikana katika utekelezaji wa mipango na majukumu ya wizara
katika mwaka uliopita.
Dkt. Rwiza aliongeza kuwa kikao hicho kimewapa watumishi nafasi
ya kujitathmini kwa kuzingatia uhalisia wa utendaji kazi na kujadili namna bora
ya kuhakikisha malengo ya wizara yanafikiwa kwa ufanisi.
Aliongeza kuwa washiriki wamepata fursa ya kutazama kwa pamoja
changamoto za rasilimali na kubaini namna ya kuongeza ufanisi ili kupata
matokeov makubwa zaidi kwa kutumia rasilimali zilizopo, huku wakielekezwa
kuimarisha mshikamano na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao
Comments
Post a Comment