NW. Salome: Wizara ya Nishati ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata Umeme wa uhakika
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema jukumu kuu la
Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika na wanapatiwa
taarifa kwa wakati pindi changamoto zinapojitokeza.
Makamba aliyasema hayo wakati akijibu swali la Exaud Kigahe, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini aliyetaka kufahamu lini serikali itabadilisha mkataba wa usambazaji wa umeme kwa wananchi kutoka Mwenga Power kwenda TANESCO, ili Mwenga Power ibaki kuwa mzalishaji wa umeme.
Akijibu swali hilo, Makamba alisema kuwa utoaji na usimamizi wa
leseni za uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini ni jukumu la kisheria la
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kwa mujibu wa Sheria ya Umeme
ya mwaka 2008 na taratibu za utoaji wa leseni hizo.
“Jukumu namba moja la Wizara ya Nishati ni kuhakikisha wananchi
wanapata umeme wa uhakika na wanapata taarifa kwa wakati kunapotokea
changamoto,” alisema Makamba.
Alieleza kuwa uamuzi wowote wa kubadili muundo wa leseni ya
usambazaji umeme katika eneo hilo unapaswa kuzingatia matakwa ya sheria na
taratibu zilizowekwa.
Hata hivyo, Makamba alisema kuwa serikali, kwa kutambua kuwa
kumekuwa na malalamiko kuhusu ubora wa huduma inayotolewa na Mwenga Power,
tayari taasisi zake za EWURA, TANESCO na REA zimeanza kufanya tathmini ya kina
ili kubaini uwezekano wa kufanya mabadiliko hayo bila kuathiri uwekezaji
uliopo.
Alisema kuwa tathmini hiyo itafanyika kwa haraka ili kuhakikisha
wananchi wanapata huduma ya umeme yenye uhakika na inayokidhi mahitaji yao.
Alisema yupo tayari, pindi vikao vya Bunge vitakapokamilika,
kuongozana na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, kwenda kusikiliza na
kufahamu kwa kina changamoto zinazowakabili wananchi katika eneo hilo.
Comments
Post a Comment