Acheni matumizi ya pombe yaliyokithiri kuepuka changamoto ya afya ya akili
Na. Hassan Kimweri, WAF - DODOMA
Serikali imewataka wananchi hususan vijana, kupunguza matumizi ya pombe yaliyokithiri na kuacha matumizi ya dawa za kulevya ili kuepuka changamoto za afya ya akili pamoja na madhara mengine kwa familia na jamii.
Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati akifungua mafunzo kwa wataalaamu wa afya ya akili yaliyofanyika mkoani Dodoma yenye lengo la kuongeza huduma za kinga na matibabu kwa waraibu.
“Matumizi ya pombe yaliyokithiri ni miongoni mwa changamoto zinazopaswa kupewa
kipaumbele, hasa kutokana na vijana kuanza kutumia pombe katika umri mdogo
ambapo hali hiyo inaweza kuathiri masomo, kazi, mahusiano ya kifamilia na uwezo
wa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za jamii” alisema Dkt. Magembe.
Alisema kuwa matumizi yaliyokithiri ya pombe na dawa za kulevya yanachangia
vitendo vya ukatili na migogoro katika jamii, huku akisisitiza kuwa mtu anapofikia
hatua ya utegemezi mkubwa wa vilevi, kumsaidia kuacha si jambo rahisi na
kunahitaji wataalamu, matibabu, muda pamoja na ushirikiano wa familia na jamii
na jamii inayomzunguka.
Alisema kuwa, serikali imeendelea kuongeza vituo vinavyotibu uraibu kutoka kituo 1 hadi vituo 14 na huduma hizo kwa sasa zinaendelea kusogezwa ngazi za chini walipo wananchi ambapo amesisitiza kuwa huduma hizi zitolewe bila unyanyapaa wala ubaguzi na kushirikiana na wamiliki wa vituo vya utengemao (Sober houses) ili kuwafikia waathirika wengi zaidi.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Huduma Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Hamadi Nyembea alisema kuwa mafunzo
hayo yatasaidia jamii kwakuwa yanakwenda kutolewa kwa wataalamu wa afya katika
mikoa 17, hususan katika maeneo yenye matumizi makubwa ya pombe.
Mwisho, alisema kuwa jukumu la wataalamu wa afya ni kuwatambua wenye changamoto mapema, kutoa huduma za awali na kuwapeleka katika vituo vya ngazi za juu pale wanapohitaji huduma za kibingwa zaidi, hatua itakayosaidia wananchi kupata huduma kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi.
Serikali
imesisitiza kuwa watu wenye changamoto za afya ya akili hawapaswi
kunyanyapaliwa wala kutengwa, bali wanapaswa kusikilizwa, kusaidiwa na kupewa
nafasi ya kurejea katika maisha ya kawaida, matibabu ya afya ya akili si dawa
pekee, bali yanapaswa kuhusisha familia, jamii na mazingira ambayo mgonjwa
anaishi.
Comments
Post a Comment