Bunge lapitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Mwaka 2026
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2026 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments)
(No. 02) Bill, 2026), tarehe 2 Septemba, 2026 katika Mkutano wa Nne, Kikao cha
Sita cha Bunge kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alisema kuwa muswada unakusudia kufanya maboresho katika Sheria kuu Saba.
“Malengo ya marekebisho haya ni kuboresha utekelezaji wa masharti ya sheria husika na kuzifanya sheria hizi ziendane na wakati na kuleta tija kwa wananchi” alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, alizitaja sheria
zilizofanyiwa marekebisho ni pamoja na Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi,
Sura ya 116, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287,
Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 na Sheria ya Baraza
la Usalama la Taifa, Sura ya 61.
Johari aliendelea kueleza
kuwa Sheria ya Mamlaka ya Nchi Katika Umiliki wa Mali na Rasilimali Asilia,
Sura ya 449, Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini, Sura ya 138, Sheria
ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283 nazo zimejumuishwa katika muswada huo.
Katika hatua
nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kuwa serikali itaendelea kufanya
maboresho katika sheria mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 inatekekelezwa ipasavyo.
“Kwa niaba ya serikali, niliahidi Bunge lako tukufu kuwa, serikali itaendelea
kufanya maboresho ya sheria ili kuhakikisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo
2050 iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu inatekekelezwa ipasavyo” alisema Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Mara baada ya Bunge
kupitisha Muswada huo, utapelekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa ajili ya kusainiwa na kuwa sheria kamili za nchi.
Comments
Post a Comment