Wananchi watakiwa kuzingatia taratibu za kupata Hati ya kusafiria Dodoma

Na. Coletha Charles, MNADANI

 

Wananchi wametakiwa kuzingatia taratibu na kuandaa nyaraka zinazohitajika wakati wa kuomba hati ya kusafiria nje ya nchi ili kurahisisha mchakato wa maombi na kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

 

Wito huo umetolewa na Afisa Uhamiaji, Constable Asia Mussa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALiKi) na Samia Day 2026, yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Jitegemee, Kata ya Mnanda, Jiji la Dodoma.

 

Alisema kuwa nyaraka zinazohitajika hutegemea shughuli za mwombaji na sababu za safari, akiwataka waombaji kuandaa vielelezo vinavyothibitisha utambulisho wao, shughuli wanazofanya na madhumuni ya safari.

 

“Ni muhimu mwombaji kuandaa nyaraka zinazohitajika kulingana na shughuli anazofanya na madhumuni ya safari yake ili kurahisisha mchakato wa maombi ya ‘passport’,” alisema Constable Mussa.

 

Alisema kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuandaa fomu ya maombi ya hati ya kusafiria, kitambulisho cha taifa, barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa na leseni ya biashara, kulingana na mahitaji ya maombi yao.

 

Aliongeza kuwa watu wanaokusudia kusafiri kwa ajili ya kumtembelea mtu wanapaswa kuandaa barua ya mwaliko kutoka kwa mwenyeji wao, barua ya utambulisho kutoka serikali ya mtaa na nyaraka nyingine zinazohitajika kuthibitisha madhumuni ya safari.

 

“Kwa upande wa wakulima na wafanyabiashara wadogo, taarifa za kifedha, ikiwamo taarifa ya akaunti ya benki, zinaweza kuhitajika kulingana na mazingira ya maombi na nyaraka zinazotakiwa kuthibitisha uwezo wa kifedha,” alisema Constable Mussa.

 

Nae mkazi wa Mtaa wa Mnadani, Gogo Mtemi alisema kuwa elimu hiyo ni muhimu katika kuwasaidia wananchi kufahamu taratibu za kuomba pasipoti na kuandaa nyaraka mapema.

 

“Elimu hii inatusaidia kuelewa umuhimu wa kuandaa nyaraka zinazohitajika kabla ya kuomba pasipoti, hivyo ni vyema kupata taarifa sahihi kutoka mamlaka husika ili kuepuka usumbufu,” alisema Mtemi.

 

Idara ya Uhamiaji imeendelea kuhimiza wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu taratibu za maombi ya hati za kusafiria kupitia mamlaka husika, ili kuhakikisha wanakamilisha mahitaji yanayotakiwa kwa wakati na kuepuka ucheleweshaji unaoweza kuzuilika.

 

MWISHO

Comments

Popular Posts

Hai DC yajifunza kuimarisha usafi na usimamizi wa taka Jiji la Dodoma

Kata ya Matumbulu wanufaika na Mil. 114.7 Maadhimisho ya Samia Day

Samia Day 2026 yaibua vipaji vya michezo Kata ya Matumbulu