KATA YA CHAMWINO YATEKELEZA AGIZO LA USAFI WA MAZINGIRA

Na. Mwandishi wetu, CHAMWINO

Wananchi wa Kata ya Chamwino, Jiji la Dodoma, wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la usafi wa mazingira kwa lengo la kuboresha mandhari ya mji na kujikinga na magonjwa yanayotokana na uchafu. Zoezi hilo limeonesha mwitikio wa wananchi katika kushirikiana kutunza mazingira na kuifanya jamii kuwa safi na salama.



Akizungumza na wananchi wakati wa zoezi hilo, Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa Taka Ngumu Jiji la Dodoma, Mkana Mkana, alisema kuwa mazingira machafu ni chanzo cha magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababisha wananchi kutumia muda na fedha nyingi kupata matibabu badala ya kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali.

Alisema kuwa usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi na kusisitiza kuwa watakaoshindwa kutekeleza wajibu huo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kutozwa faini ya shilingi 300,000 pamoja na kifungo kwa mujibu wa sheria. Alitoa wito kwa wananchi kufanya usafi kila siku ili kujikinga na magonjwa na kuboresha afya zao.

Kwa upande wake, Mariam Swedi, mkazi wa Kata ya Chamwino, alisema kuwa amefurahishwa na mwitikio wa wananchi katika zoezi hilo, akieleza kuwa kufanya usafi mara kwa mara kunasaidia kuboresha mazingira ya makazi na kupunguza hatari ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu.



Nae Saidi Rajabu, mkazi wa Chamwino na mfanyabiashara katika Soko la Bonanza, alisema kuwa hali ya usafi imeimarika kutokana na ushiriki wa wananchi. Aliipongeza serikali kwa kuhamasisha zoezi hilo na kueleza kuwa usafi ni muhimu hasa baada ya mvua zinazoacha taka na uchafu unaoweza kuathiri shughuli za wafanyabiashara.

Wananchi wametakiwa kuendeleza mwamko huo kwa kufanya usafi katika maeneo yao ya makazi na biashara kila siku, badala ya kusubiri kuhamasishwa, ili kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi, salama na lenye mazingira bora kwa wote.

 




Comments

Popular Posts

MABARAZA YA ARDHI YANAMCHANGO KATIKA KUSULUHISHA MIGOGORO YA ARDHI

Mwenyekiti UWT Taifa awataka wanawake kuchangamkia mikopo ya Jiji la Dodoma