Wakazi Mtaa wa Mazengo wapatiwa elimu ya Lishe
Na. Ramadhani Mohammed, ZUZU
Wakazi wa Mtaa wa Mazengo, Kata ya Zuzu jijini Dodoma,
wamepatiwa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto, ikiwa ni sehemu ya
kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ulaji wa vyakula vyenye virutubishi muhimu kwa
ukuaji na maendeleo ya watoto.
Akizungumza baada ya kupata elimu hiyo, mkazi wa Mtaa wa Mazengo, Dorice Robert Mwibala alisema kuwa elimu hiyo imewasaidia kufahamu mambo mbalimbali ambayo awali hawakuwa wakiyajua kuhusu lishe ya watoto, huku akieleza kuwa itakuwa na manufaa kwa watoto na wajukuu wao.
Alisema kuwa elimu hiyo imewafurahisha kwa kuwa imewapa
uelewa muhimu kuhusu namna ya kuzingatia lishe bora kwa watoto, jambo analoona
linaweza kusaidia kuboresha afya na maendeleo yao.
Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma, Ibrahimu Mgeni alisema
kuwa elimu hiyo atawafikishia watu wake wa karibu ili nao waweze kufahamu
umuhimu wa lishe bora, huku akiomba elimu kama hiyo iendelee kutolewa mara kwa
mara katika jamii.
Mgeni alisema kuwa hakuna jambo bora kwa mtoto kama kupata lishe bora, akieleza kuwa watoto wanaopata lishe nzuri, wakiwemo wanafunzi wa darasa la awali, huwa katika mazingira mazuri ya kujifunza na kupokea yale wanayofundishwa darasani.
Nae Mtendaji wa Mtaa wa Mazengo, Erick Masima aliitaka jamii
kuwa na utaratibu wa kujitokeza kwa wingi katika shughuli zinazolenga kutoa
elimu ya lishe, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika
kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi na kuchangia ustawi wa watoto.
Comments
Post a Comment