Jukwaa la mifumo ya chakula lazinduliwa Dodoma

Na. Rahma Magona, DODOMA

 

Jukwaa la Mifumo ya Chakula Halmashauri ya Jiji la Dodoma limezinduliwa leo katika Hoteli ya Mesuma jijini Dodoma, likiwa na lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano wa wadau katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora na salama kwa wananchi.

 


Akizungumza katika uzinduzi huo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, alisema kuwa jukwaa hilo litakuwa chombo cha uratibu kitakachowaunganisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana maarifa, uzoefu na rasilimali, pamoja na kutafuta suluhisho endelevu za changamoto zinazoweza kujitokeza katika mfumo wa chakula.

 

Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea kukua kwa kasi, hali inayoambatana na ongezeko la mahitaji ya chakula bora na salama, huku mfumo wa chakula ukitegemea uzalishaji kutoka katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Mbeya, Iringa na Morogoro.

 


Chaula alisisitiza kuwa changamoto katika mfumo wa chakula inahusisha mnyororo mzima kuanzia uzalishaji, usafirishaji, usindikaji, masoko hadi matumizi ya chakula, hivyo jukwaa hilo litasaidia wadau kushirikiana katika kuzitafutia suluhisho endelevu.

 

Alisema kuwa mafanikio ya jukwaa hilo yanategemea ushirikiano wa kila mdau, huku serikali ikiahidi kutoa ushirikiano na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta mbalimbali katika kuhakikisha lengo la kuwa na chakula bora na salama kwa wananchi wa Jiji la Dodoma linafikiwa.

Comments

Popular Posts

Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari

Jiji la Dodoma Biashara saa 24, usafi saa 24

Wananchi Dodoma wahimizwa kufanya usafi wa Mazingira kila siku