Meya Chaula azindua Jukwaa la Mfumo wa Chakula Jiji la Dodoma

Na. Mwandishi wetu, DODOMA

 

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, amezindua rasmi Jukwaa la Wadau wa Mfumo wa Chakula katika Jiji la Dodoma kupitia Mradi wa ‘Growing Together’ unaotekelezwa na Taasisi ya Rikolto, kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali na kujadili namna ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama na chenye lishe katika Jiji la Dodoma.

 


Uzinduzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Mesuma, umewakutanisha wadau mbalimbali wa mfumo wa chakula, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wawakilishi wa makampuni mbalimbali, taasisi na wadau wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwa ajili ya kujadili kwa pamoja fursa na changamoto zinazohusu uzalishaji, upatikanaji na uhifadhi wa chakula.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Meya Chaula alisema kuwa masuala ya mfumo wa chakula hayawezi kutekelezwa na mtu mmoja, bali yanahitaji ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wengine, hususan kutokana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma inayoongeza mahitaji ya chakula salama na chenye lishe.

 

“Masuala ya mfumo wa chakula hayawezi kufanywa na mtu mmoja, bali yanahitaji ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi. Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Taasisi ya Rikolto kupitia Mradi wa Growing Together tumezindua jukwaa hili litakalowakutanisha wadau mbalimbali wa mfumo wa chakula, na Halmashauri itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha Jiji la Dodoma linapata chakula salama na chenye lishe” alisema Chaula.

 


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Rikolto Afrika Mashariki, Kain Mvanda, alisema kuwa miji inayokua kwa kasi hukumbwa na ongezeko la watu na mahitaji ya chakula huongezeka hivyo ni muhimu kwa wadau kukutana na kujadili namna bora ya kuboresha uzalishaji, utunzaji na usalama wa chakula. Alisema jukwaa hilo litasaidia kuimarisha ushirikiano na kuleta pamoja wadau mbalimbali wa chakula.

 

Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa mfumo wa chakula, kwa lengo la kuboresha uzalishaji na kuhakikisha chakula salama na chenye lishe kinapatikana kwa wananchi wa Jiji la Dodoma.

Comments

Popular Posts

Jiji la Dodoma Biashara saa 24, usafi saa 24

Mvua za El Nino: DC Shekimweri awaasa wananchi wa Dodoma Kuchukua Tahadhari

Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Wilaya ya Dodoma lapata viongozi wapya kwa miaka mitatu