Mkuu wa Wilaya Dodoma aagiza ujenzi Fensi maeneo ya wazi Nkuhungu
Na. Mwandishi wetu, NKUHUNGU
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri,
ameagiza maeneo yote ya wazi katika Kata ya Nkuhungu kuwekwa fensi ili
kuyakinga dhidi ya uvamizi na matumizi yasiyo sahihi, ikiwemo uuzaji holela wa
maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya umma.
Alhaj Shekimweri alitoa agizo hilo alipofanya ziara katika Mtaa wa Bochela kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabwawa yanayolenga kudhibiti maji ya mvua na kupunguza athari za mafuriko katika makazi ya wananchi.
Alisema kuwa ulinzi wa maeneo ya wazi ni muhimu katika
kuhakikisha yanabaki kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuzuia watu kuyavamia au
kuyagawa na kuuziana kinyume cha taratibu, hali ambayo inaweza kuathiri mipango
ya maendeleo kwa siku zijazo.
“Kila eneo la wazi katika kata hii liwekewe fensi ili
kuzuia uvamizi na watu kuuziana maeneo ya wazi, hali ambayo inaweza kuleta
changamoto baadaye,” alisema Alhaj Shekimweri.
Aidha, alisema kuwa uwekaji wa fensi utasaidia kulinda maeneo hayo pamoja na miundombinu inayotekelezwa kwa ajili ya kudhibiti maji, ili ibaki salama na itumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Aliagiza hatua hiyo izingatiwe katika maeneo yote ya
wazi ya kata hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda maeneo ya umma kwa
manufaa ya wananchi na maendeleo ya eneo hilo.


Comments
Post a Comment