DC Dodoma atembelea mradi wa mabwawa Nkuhungu
Na. Mwandishi wetu, NKUHUNGU
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri,
ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa mabwawa katika Kata ya
Nkuhungu, unaotekelezwa katika Mitaa ya Bochela, Mtube, Salama na Mnyakongo kwa
lengo la kudhibiti changamoto ya mafuriko katika maeneo ya makazi.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa mabwawa yatakayosaidia kudhibiti na kuelekeza maji ya mvua katika maeneo yaliyotengwa, hatua inayolenga kupunguza maji kujaa katika makazi ya wananchi wakati wa mvua kubwa.
Aidha, mabwawa hayo yanatarajiwa kuunganishwa na mfumo
wa mabwawa pamoja na visima vilivyopo katika mitaa hiyo, ili kuwezesha udhibiti
mzuri wa mtiririko wa maji na kupunguza athari za mafuriko.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya
Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, alisema kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza athari za mafuriko na kuwawezesha wananchi kuendelea na
shughuli zao za kila siku kwa usalama.
Aliwataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati, hususan kabla ya kuanza kwa mvua kubwa zinazoweza kuongeza hatari ya mafuriko katika maeneo hayo.
Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi
kwa wakati kutasaidia miundombinu hiyo kuanza kutumika mapema na hivyo
kupunguza athari za mafuriko pamoja na kulinda usalama na mali za wananchi wa
Kata ya Nkuhungu.


Comments
Post a Comment