DC Shekimweri azitaka Kamati za Maafa ngazi ya Kata kutoa elimu kwa wananchi
Na. Mwandishi wetu, NKUHUNGU
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri,
amezitaka Kamati za Maafa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari
na hatua za kuchukua mapema ili kujikinga na athari zinazoweza kusababishwa na
mafuriko.
Alhaj Shekimweri alitoa kauli hiyo baada ya kuipongeza Kamati ya Maafa ya Kata ya Nkuhungu kwa jitihada inazoendelea kufanya katika kuwaelimisha wananchi na kuhakikisha wanajiandaa kukabiliana na changamoto za mafuriko.
Alisema kuwa ni muhimu kamati hizo kutowasubiri
wananchi hadi maafa yatokee, bali ziendelee kutoa elimu na kuchukua hatua za
tahadhari mapema, hususan kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayoweza
kuathiriwa na mafuriko.
Aidha, alizitaka kamati hizo kuwasaidia wananchi
wanaoishi katika maeneo hatarishi kuhamia maeneo salama. Alisema kuwa pale
inapowezekana, wananchi hao wanaweza kuunganishwa na ndugu zao kwa muda wakati
hatua nyingine za kupata maeneo salama ya kuishi zikiendelea kuchukuliwa.
“Tusisubiri maafa yatokee ndipo tuanze kuchukua hatua.
Ni muhimu wananchi waelimishwe mapema na wale walio katika maeneo hatarishi
wasaidiwe kuhamia maeneo salama,” alisema Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nkuhungu, Julius Ezekiel alisema kuwa wamepokea maelekezo hayo na wataendelea kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na kamati pamoja na wananchi, ili kuhakikisha usalama wao unalindwa na wanaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.


Comments
Post a Comment