DC Shekimweri aagiza kusafisha mitaro kukabili Mvua za El Nino
Na. Mwandishi wetu, DODOMA
TANROADS, TARURA na wananchi wameagizwa kushirikiana
kusafisha mitaro, makalavati na njia za maji katika maeneo hatarishi,
Kukabiliana na mvua kubwa zinazotarajiwa za El Nino na kuzuia mafuriko.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri wakati akikagua maeneo mbalimbali yanayoweza kuathiriwa na mvua kubwa katika Kata za Nzuguni, Makole, Ipagala na Kiwanja cha Ndege Jiji la Dodoma.
Alisema kuwa maandalizi ya mapema ni muhimu katika
kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo mafuriko, maji
kutuama, kuharibika kwa miundombinu pamoja na kuathiri makazi na shughuli za
wananchi.
Shekimweri alisema kuwa usafishaji wa mitaro mikubwa
unapaswa kufanyika kwa wakati, huku taka, udongo na vitu vingine vinavyoweza
kuzuia mtiririko wa maji vikiondolewa kabla mvua kubwa hazijaanza.
“Ni muhimu kufanya maandalizi mapema badala ya kusubiri mvua zianze. Mitaro mikubwa lazima isafishwe na maeneo ambayo yana changamoto yatambuliwe ili hatua zichukuliwe kwa wakati,” alisema Alhaj. Shekimweri.
Alisisitiza kuwa taasisi zinazohusika zinapaswa
kufanya kazi kwa ushirikiano, kuhakikisha mitaro, makalavati na njia za maji
zinakuwa katika hali inayowezesha maji kupita kwa urahisi wakati wa mvua.
Aidha, aliwataka wananchi kuacha kutupa taka kwenye
mitaro na njia za maji, akisema tabia hiyo inaweza kuziba mifumo ya maji na
kuongeza hatari ya mafuriko.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kufuatilia maeneo
yenye changamoto na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa wakati, huku
wananchi wakitakiwa kushiriki katika usafi wa mazingira na kutoa taarifa kuhusu
maeneo yanayohitaji uingiliaji wa haraka.
Ziara hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa, kwa kuimarisha mifumo ya maji na kuhakikisha maeneo hatarishi yanachukuliwa hatua kabla ya mvua kuanza.



Comments
Post a Comment